Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Bw. Deodatus Balile
…………………………………………………………
Benedict Liwenga- WHUSM
WADAU wa Habari wameisifu Serikali kwa kuundaa na kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za Jabari.
Wamesema ni jambo ambalo lilikuwa
limesubiriwa kwa muda mrefu tangu mchakato ulipoanza miaka ya 80 na
baadaye kuzimika halafu na kurudi tena miaka ya hivi karibuni hususani
mwaka juzi na mwaka jana 2015.
Akiongea kupitia kituo kimoja cha
cha Televisheni nchini jana, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri na
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini, Bw. Deodatus Balile
amesema amefurahishwa sana na Muswada huu kuwataka wanahabari
kujiendeleza kitaaluma jambo ambalo amesema ni muhimu katika taaluma
yoyote.
“Kwa kweli kuhusu Mwandishi wa
habari kusoma au kuwa na digrii, hili naliunga mkono, inabidi waandishi
wasome na kama hawataki kusoma basi wajaribu ujinga”, alisema Balile.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya
Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Hassan Abbas amesema
kuwa Muswada huu ni muhimu kwa wanahabari na taaluma ya habari kwa
ujumla kwani ni kwa mara ya kwanza katika Tanzania uandishi wa habari
unaenda kuwa taaluma.
“Nipende kuwaasa wana taaluma
wenzangu kuusoma Muswada huu na kutoa maoni badala ya kulalamika kwani
sisi ndiyo tunaoielewa zaidi taaluma ya habari, hivyo maoni yetu ni
muhimu”, alisema Abbas.
Abbas aliongeza kuwa, Muswada huo
utafanya uandishi wa habari kuwa taaluma inayoheshimika na utaanzisha
Baraza Huru la Habari na Bodi ya Ithibati ya wanahabari, mambo ambayo
yamekuwa yakipiganiwa na wanahabari. Hivyo Muswada huu ni wa manufaa kwa
wanahabari.
Akiongea katika ziara maalum
aliyofanya Mkurugenzi wa MAELEZO katika ofisi za Majira, Mhariri
Mtendaji wa Majira, Bwana Emmnanuel Mbuguni alisema kwamba amefurahishwa
na kipengele cha wanahahabari kusoma ili kuongeza weledi katika kazi
yao. Hivyo, amesema kwa jinsi hiyo anakubaliana na Muswada huo na
akaahidi kutoa maoni yake zaidi kupitia barua pepe ya Bunge.
Muswada wa Sheria ya Huduma za
Habari umewasilishwa Bungeni mwezi Septemba mwaka huu na baadaye wadau
wakaruhusiwa kutoa maoni yao kwenye muswada huo kabla ya kusomwa kwa
mara ya pili mapema mwezi ujao yaani Novemba.
Tags
HABARI KITAIFA