| mmoja wa wafanyabiashara katika kituo cha daladala jamatini akifafanua jambo wakati alipokuwa akiuliza swali kwa mkurugenzi wa manispaa kuhusu kutakiwa kusaini mkataba wa pili yaani wa Manispaa na Rahco
Na RAMADHAN
HASSAN
-DODOMA
SINTOFAHAMU
imewakumba wafanyabiashara katika stendi za Jamatini,Mkoa na eneo la Sarafina licha ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma
kuahidi kuwa atawasimamia ili waendelea kufanya biashara hadi watakapotafutiwa
eneo mbadala.
Sintofahamu hiyo
imekuja baada ya Uongozi wa Kampuni hodhi ya mali za Railway (Rahco) kutaka
wafanyabiashara wa maeneo hayo waondoke kwa madai ya kutaka kuanzisha
ujenzi wa reli ya standard geji.
Kutokana na hali
hiyo jana Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi, alifika katika
maeneo hayo na kuzungumza na wafanyabiashara huku akiwasihi kutulia wakati
serikali ikiendelea kulifanyia kazi suala lao.
Kunambi alisema
tayari alishafikisha kilio chake kwa Rahco na uongozi wa mkoa ili Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) waende kuwaonyesha mipaka halisi ya eneo hilo na
kutambua wangapi wako ndani ya eneo la Rahco na wangapi watakuwa chini ya
Manispaa.
“Najua kuwa mnasumbuliwa, lakini naomba
tupeane siku saba hapa ili kusudi tuweze kufanya kazi vizuri, Mkuu wa mkoa
ameamua kutukutanisha sisi Manispaa, CDA na wenzetu wa Rahco ili kwa pamoja
tuweze kuzungumzia jambo hilo, hivyo vuteni subira,” alisema Kunambi.
Awali mwenyekiti
wa soko la Jamatini John Banda alisema wafanyabiashara wa maeneo hayo wamekuwa
na hali ya sintofahamu kwani Rahco ilishatishia kuwabomolea vibanda vyao pamoja
na kuwataka wasaini mikataba kwa haraka.
Banda alisema
Rahco wamewapa mikataba wafanyabiashara ili waisaini kabla ya Desemba 31 na
wasipofanya hivyo wahesabu wamejiondoa na huenda wakaondolewa kwa nguvu.
Mfanyabiashara
Mwajuma Issa alisema shida wanayoipata katika maeneo hayo ni kwa sababu
Manispaa ya Dodoma ipo kama nchi inayoelea angani kwa kukosa ardhi chini.
Mwajuma
alibainisha kuwa kama Manispaa ingekuwa na ardhi yake bila ya kuingiliwa na CDA
huenda mambo yote hayo yasingelitokea kwa wakati huu kwani mpango ungewekwa
mahususi kwa ajili kuwasaidia wafanyabiashara.
mwisho
|