Aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Charles Boniface
Mkwasa Jumanne hii ametangazwa rasmi kuwa Katibu Mkuu wa Yanga.
Mkwasa mwenye taaluma ya ukocha daraja la kwanza la CAF, amewahi
kuzifundisha klabu mbalimbali ikiwemo Yanga kwa vipindi tofauti na timu
za taifa za wanaume na wanawake.
Kabla ya hapo, Mkwasa alikuwa kocha wa timu ya Taifa Stars kwa kipindi
cha miezi 17 kabla ya TFF kusitisha mkataba wake mapema Januari 2017.
Makamu mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga amemtambulisha Mkwasa
leo mbele ya waandishi wa habari na kusema kocha huyo ambaye pia ni
mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, ameingia mkataba wa miaka miwili.
Mkwasa anachukua nafasi ya Baraka Deusdedit aliyekaimu nafasi hiyo kwa
kipindi cha mwaka mmoja, kufuatia kuondoka kwa Jonas Tiboroha mapema
mwanzoni mwa mwaka jana.
“Kwa niaba ya uongozi mzima wa Yanga Sc namtangaza rasmi sasa Boniface
Mkwasa mchezaji wetu na mwalimu wetu wazamani kuwa ndie katibu mkuu mpya
wa klabu yetu ya Yanga Sc”
Tags
MICHEZO KITAIFA
