MTU mmoja mwanaume ambaye amejulikana kwa jina moja la Mungiki (35)
ameuawa kwa kupigwa na risasi na askari polisi wakati akijaribu
kuwatoroka baada ya kukutwa akiwa na silaha aina ya bastola yenye namba
za usajili TZCAR 97076.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi alisema jana kuwa tukio
hilo lilitokea Januari 27, mwaka huu saa 6.30 usiku katika Mtaa wa
Bwiru Kata ya Kitangiri katika Manispaa ya Ilemela.
Alisema bastola aliyokamatwa nayo aliipora kwenye tukio la unyang’anyi
wa kutumia silaha mwaka 2013 mkoani Tabora. Alisema polisi walipata
taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo kwa kijana anayejihusisha
matukio ya uhalifu wa kutumia silaha jijini Mwanza na mikoa jirani.
“ Polisi walifanya ufuatiliaji wa tukio hilo, na kufanikiwa kumkamata
mtuhumiwa na baada ya kuhojiwa alikiri kuwa na silaha hiyo na ndipo
alipowaongoza askari hadi maeneo ya Songambele mtaa wa Kabohoro kwenye
mapango ya mawe na kuikuta bastola hiyo ikiwa imefichwa kwenye pango la
jiwe,” alifafanua.
Alisema mtuhumiwa alikiri kupewa bunduki na mtu mmoja ( jina
limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama) ambaye walikuwa wakishirikiana
kwenye matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha jijini Mwanza
na mikoa jirani.
Alisema mtuhumiwa alisema walishirikiana na mwenzake huyo katika kuvamia
kwenye maduka mawili yanayofanya miamala ya fedha katika maeneo ya
Kilimahewa kwa Msuka na kupora vitu mbalimbali kwa kutumia silaha hiyo
na kufunguliwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha yenye namba
MZN/IR/632/2017.
“Askari waliongozana hadi kwenye alikokuwa ameficha silaha, lakini
ghafla mtuhumiwa alikurupuka akiwa na pingu mkononi na kuanza kukimbilia
upande wa pili wa barabara kwa lengo la kutoroka. “Askari walifyatua
risasi kadhaa hewani wakimuamuru asimame lakini alikaidi na ndipo
walifyatua risasi wakimlenga kwenye miguu lakini kwa bahati ilimpiga
sehemu za juu za kiuno, ambapo mtuhumiwa alikufa akiwa njiani kuelekea
hospitalini,” alifafanua.
Tags
HABARI KITAIFA
