RAIS John Magufuli ameondoka nchini na kuelekea Addis Ababa, Ethiopia
ambako atahudhuria Mkutano Kilele wa 28 wa Wakuu wa Nchi wanachama wa
Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea nchini humo.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Rais Magufuli kutoka nje ya nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) tangu aingie madarakani kuongoza Serikali ya
Awamu ya Tano Novemba 5, mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu Dar es Salaam jana ilisema katika Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wa jijini Dar es Salaam, Rais
Magufuli aliagwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa.
Wengine waliojumuika kumuaga Rais Magufuli ni viongozi mbalimbali wa
Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Dar es Salaam, pamoja na kuhudhuria mkutano huo,
akiwa Addis Ababa, Rais Magufuli anatarajiwa kukutana na kufanya
mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Bara la Afrika wanaohudhuria
mkutano huo.
Tags
HABARI KITAIFA
