WAKATI Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) likitangaza matokeo ya Kidato
cha Nne kwa mwaka 2016 na kuonesha ufaulu wa jumla kwa watahiniwa wa
shule umeongezeka kwa asilimia 2.44, idadi ya watahiniwa waliopata alama
za kuwawezesha kuendelea na kidato cha tano imekuwa chini kwa miaka
mitatu mfululizo.
Matokeo ya mtihani uliofanyika Novemba, 2016 na kutangazwa jana jijini
Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, yanaonesha
watahiniwa wa shule 244,762 ambayo ni asilimia 70.35 ya waliofanya
mtihani walifaulu mtihani huo.
Ufaulu huo unaonesha kuongezeka kwa asilimia 2.44 ukilinganisha na
matokeo ya mwaka 2015 ambayo wanafunzi 240,996 ambao ni asilimia 67.91
walifaulu na kwa mwaka 2014 walikuwa ni 169,642 (asilimia 69.76) na
mwaka 2013 walikuwa ni 201,152 ambao ni asilimia 57.09.
Jumla ya watahiniwa 408,372 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha
nne mwaka 2016, wakiwemo wasichana 209, 456 sawa na asilimia 51.29 na
wavulana 1998, 916 (asilimia 48.71).
Kati yao wote waliosajiliwa, watahiniwa wa shule walikuwa 355,822 na wa
watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,550. Ufaulu kwenda Kidato cha V
Pamoja na ufaulu huo kuongezeka, inaonesha kuwa watahiniwa wanaopata
madaraja yanayoweza kuwafanya wakaingia kidato cha tano (daraja la
I-III), inaonekana kuwa chini ya asilimia 50.
Kwa matokeo ya mwaka jana, watahiniwa 96.018 ambao ni asilimia 27.60
wamepata daraka la I-III, wakati mwaka 2015 walikuwa ni 89,929 ambayo ni
asilimia 25.34 na mwaka 2014 walikuwa ni 73,832 ambao ni asilimia
30.72.
Watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 32,521 sawa na asilimia
68.19. mwaka 2015 walikuwa ni 31,1951 sawa na asilimia 64.80, hivyo
ufaulu kuongezeka kwa asilimia 3.39. Kwa upande wa maarifa, watahiniwa
8,751 sawa na asilimia 50.48 wamefaulu, mwaka 2015 watahiniwa 7,536
ambao ni asilimia 46.63 hivyo kuwapo ongezeko ya ufaulu kwa asilimia
3.85.
Kuhusu ufaulu wa masomo unaonesha kuwa masomo ya Historia, Jiografia,
Kiswahili, Kiingereza, Hisabati, Fizikia, Biolojia, Commerce na
Book-Keeping umepanda kwa asilimia 0.12 na asilimia 8.08 ikilinganishwa
na mwaka 2015.
Watahiniwa wanaonekana kufanya vizuri zaidi kwenye somo la Kiswahili
ambapo ufaulu wake ni asilimia 77.75 ya watahiniwa wote, ingawa ufaulu
huo umeonekana kushuka ukilinganisha na mwaka 2015 uliokuwa ni asilimia
77.63 na mwaka 2014 ulikuwa asilimia 69.66.
Aidha, watahiniwa wameshindwa kufanya vizuri katika somo la Hisabati
ambalo pamoja na kuonekana ufaulu umeongezeka waliofaulu somo hilo ni
asilimia 18.12 ya watahiniwa wote wa shule, mwaka 2015 walikuwa ni
asilimia 16.76 na mwaka 2014 ilikuwa ni asilimia 19.58.
“Pamoja na asilimia ya ufaulu wa jumla kuendelea kuimarika, takwimu
zinaonesha kuwa bado ufaulu wa masomo na watahiniwa waliopata daraja la
I-III ni chini ya asilimia 50, hivyo juhudi za makusudi zinahitajia
kuendelea kufanya ili kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo na kuongezeka
kwa idadi ya watahiniwa kwenye madaraja ya ufaulu,” alisema Dk Msonde.
Shule za binafsi vinara
Kuhusu upangaji wa matokeo kwa shule zenye wanafunzi zaidi ya 40,
unaonesha shule za watu binafsi na mashirika ya dini zimeendelea kufanya
vizuri katika nafasi za 10 bora kitaifa huku zile zinazomilikiwa
serikali zikiendelea kufanya vibaya kwa miaka mitatu mfululizo.
Shule 10 Bora ni Feza Boys (Dar es Salaam), St Francis Girls (Mbeya),
Kaizirege Junior (Kagera), Marian Girls, Marian Boys na St Aloysius
Girls (Pwani), Shamsiye Boys (Dar es Salaam), Anwarite Girls
(Kilimanjaro), Kifungilo Girls (Tanga) na Thomas More Machrina (Dar es
Salaam).
Aidha, Mkoa wa Dar es Salaam umezorota kielimu baada ya kuwa na shule
sita kati ya 10 zilizoshika nafasi za mwisho. Shule hizo ni Kitonga na
Nyeburu (Dar es Salaam), Masaki (Pwani), Mbopo, Mbondole na Somangila
Day (Dar es Salaam), Dahani (Kilimanjaro), Ruponda (Lindi), Makiba
(Arusha) na Kidete (Dar es Salaam).
Mikoa iliyofanya vizuri katika nafasi ya 10 bora ni Njombe, Iringa,
Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Tabora
wakati halmashauri 10 bora ni Bukoba Mjini, Njombe Mjini, Kakonko,
Kahama Mji, Wanging’ombe, Ilemela, Iringa Mjini, Mkuranga, Igunga na
Kibaha Mji.
Ufaulu kwa watahiniwa 10 bora waliofanya vizuri kitaifa unaonesha kuwa
ni asilimia 50-50 kwa wavulana na wasichana huku mwaka 2016 wakiongozwa
na mvulana. Mwaka 2015, watahiniwa wa kike walikuwa ni wanne na wavulana
sita na mwaka 2014 walikuwa na uwiano sawa, lakini waliongozwa na
mwanafunzi wa kike.
Mvulana aongoza, msichana achomoza
Kwa 2016, watahiniwa 10 bora ni Alfred Shauri (Feza Boys), Cynthia
Mchechu (St Francis Girls), Erick Mamuya (Marian Boys), Jigna Chavda (St
Mary Goreti), Naomi Tundui (Mariam Girls), Victoria Chang’a (St Francis
Girls), Brian Johnson (Marian Boys), Esther Mndeme (St Mary’s Mazinde
Juu), Ally Koti (ALCP Kilasara) na Emmanuel Kajege (Marian Boys).
Watahiniwa wasichana 10 bora ni Cynthia, Jigna, Naomi, Victoria, Esther,
Christa Edward (St Francis Girls), Nelda John (Marian Girls), Mariana
Shabani (Kifungilo Girls), Beatrice Mwella (St Mary’s Mazinde Juu) na
Rachel Kisasa (Canossa).
Wavulana 10 bora kitaifa ni Alfred, Erick, Brian, Ally, Emmanuel, John
Ng’hwaya (Nyegezi Seminary), Clever Yohana (Livingstone Boys Seminary),
Desderius Rugabandana (Morning Star), Kennedy Boniface na Assad Msangi
(Feza Boys).
126 wafutiwa, 40 matokeo yazuiwa
Katika hatua nyingine, Dk Msonde alisema Necta limezuia matokeo ya
watahiniwa 33 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani
katika baadhi ya masomo, pia matokeo ya watahiniwa 124 waliopata
matatizo ya kiafya na kufanya masomo yote, watahiniwa wamepewa fursa ya
kufanya mitihani wa Kidato cha Nne 2017.
Alisema pia baraza limezuia matokeo ya wanafunzi 40 wa Shule ya
Sekondari ya Hellens wanaodaiwa alama endelevu hadi hapo mkuu wa shule
atakapowasilisha alama hizo huku likifuta matokeo ya watahiniwa 126
waliobainika kufanya udanganyifu akiwamo mmoja aliyeandika matusi katika
karatasi ya majibu.
Kati ya waliofutiwa matokeo 58 ni wa kujitegemea na 58 ni wa shule, 10
watihani wa maarifa. Mvulana kinara anena Akizungumza na gazeti hili,
mwanafunzi bora kitaifa, Alfred Shauri alisema siri ya mafanikio yake ni
bidii na kumtanguliza Mungu.
Alfred ambaye pia amefanya vizuri kwenye insha ya Afrika Mashariki
alisema: “Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kufikia ndoto yangu ya
kufanya vizuri na nitaendelea kufanya bidii kwenye masomo, ingawa
kufanya vizuri kidato cha nne haikupi njia ya kufanya vizuri kwenye
mitihani ya elimu ya juu kama hujitumi.”
Kijana huyo ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne,
anasema pamoja na wazazi wake kumtaka kufanya masomo ya sayansi ili kuwa
mhandisi, ingawa anapenda fani hiyo, lakini angependa kujikita zaidi
katika kuwekeza kwenye biashara na ujasiriamali. Mama yake Alfred, Adela
Shauri pamoja na kumpongeza mwanawe, alisema mtoto wake ni kijana
mwenye upendo na huruma ambaye anapenda kujibidisha kwenye masomo au kwa
kile anachikifanya.
“Yaani mpaka nimetetemeka niliposikia haya matokeo, lakini niseme ni
mtoto mwenye bidii katika masomo na anayemtangulia Mungu katika kila
jambo. Niwaombe wazazi wenzangu kuhakikisha tunawalea watoto wetu wakiwa
na hofu ya Mungu, kwani peke yetu hatutaweza,” alisema.
Kwa upande wa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya pili kitaifa na akiwa ni
mwanafunzi bora kwa upande wa wasichana, Cynthia Mchechu alisema: “Mpaka
sasa siamini haya matokeo, natamani kama nikalale hivi. Lakini
nashukuru sana Mungu, kwani bidii katika masomo ndiyo imemfanya kufikia
hapo.”
Msichana bora haamini
Cynthia anawashauri wanafunzi wenzake kuhakikisha wanatimiza ndoto zao
kwa kujibidiisha na kuhakikisha wanakamilisha kile wanachotaka kupata
katika maisha.
Naye Mercy Mchechu, mama mzazi wa Cynthia ambaye ni mtoto pekee wa kike
kwake na mumewe Nehemia Mchechu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC), anasema mwanawe amekuwa na juhudi ya masomo tangu akiwa
anasoma shule ya awali na msingi Rightway ya Dar es Salaam ambayo yeye
ndiye mkurugenzi wake.
“Ni binti ambaye ana bidii katika masomo na ana uwezo wa kutambua kile
anachokitaka maishani na akaweza kutekeleza,” alisema Mercy.
Tags
ELIMU
