Polisi jana waliingilia mvutano ndani ya Kanisa la Anglikana baada ya
kumzuia Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa
kushiriki ibada ya kumsimika askofu mpya wa Dayosisi ya Lweru.
Askofu Mokiwa amekuwa katika mvutano na Askofu Mkuu wa Anglikana
Tanzania, Dk Jacob Chimeledya tangu alipotangaza kumvua uongozi wa
Dayosisi ya Dar es Salaam, akidai mkuu huyo hakufuata utaratibu na
kwamba hana mamlaka ya kuchukua uamuzi huo.
Askofu Mokiwa aliwasili makao makuu ya Dayosisi ya Lweru mjini Muleba
mkoani Kagera juzi jioni na jana alitarajiwa kuungana na maaskofu
wengine kumsimika Godfrey Mbelwa kuwa askofu mpya wa dayosisi hiyo.
Lakini taarifa zilizopatikana asubuhi zilisema Askofu Mokiwa
alichukuliwa na polisi na kuhojiwa katika kituo cha Muleba, kutokana na
kuhofu kuwa kuwapo kwake kungeweza kusababisha vurugu katika ibada
iliyokuwa iongozwe na Dk Chimeledya kutokana na mvutano uliopo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi aliliambia Gazeti la
Mwananchi kuwa, jeshi hilo halikumkamata Askofu Mokiwa na kumhoji,
badala yake alisema walichukua hatua haraka baada ya kupata taarifa za
kiintelijensia kuhusu masuala ya usalama.
“Ni wajibu wetu kufuatilia. Tulimuonya; kuhusu suala la kuhudhuria au kutohudhuria, huo utakuwa ni uamuzi wake,” alisema Ollomi.
Kamanda Ollomi alisema walimuita Askofu Mokiwa juzi saa moja usiku kwa
ajili ya kumpa ushauri wa kutohudhuria sherehe hizo kwa kuwa mgogoro
uliopo katika kanisa hilo ungeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Tags
HABARI ZA DINI