BILA shaka u-mzima wa afya, kaka yangu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda. Pole kwa shughuli nzito ya ujenzi wa Taifa uliyonayo. Mimi
ndugu yako ni mzima wa afya, namshukuru Mungu. Naendelea kupambana
kwenye eneo langu,
Ndugu yangu leo nimekukumbuka kwa barua. Nimeona si vyema vuguvugu hili
la madawa ya kulevya likapita hivihivi bila mimi kuzungumza jambo na
wewe. Kwanza nakupongeza. Umeonesha uthubutu wa hali ya juu.
Kwa vijana wa mtaani wanasema umejilipua. Si siri inahitaji ujasiri
mkubwa sana kufanya jambo unalolifanya, ndiyo maana wengi wetu tumekuwa
tukiishia kusema tu chinichini kwamba fulani anauza, fulani anatumia
madawa ya kulevya lakini si hadharani.
Ndugu yangu mimi naona kwa ulichokifanya, kinapaswa kuungwa mkono na mtu
yeyote kwa kuwa dhamira yako ilikuwa njema. Hata kama watu wameibuka na
kukupinga, kuibua ‘madudu’ wanayoyajua lakini mwisho wa siku lazima
tukubaliane tu, wewe umeonesha kwa vitendo kwamba unapaswa kuwa
kiongozi.
Vita uliyoiingia, imewashinda wengi. Hawa ambao wanaibuka sasa hivi na
kukosoa mfumo unaotumia, wengi wao walikuwa wanafahamu madhara ya madawa
ya kulevya lakini kwa sababu wanazozijua, walifunga midomo yao. Mbunge
wa Geita vijijini, Joseph Kasheku Msukuma (CCM) yawezekana alikuwa na
hoja zake za msingi katika kukukosoa, lakini niliona ni vyema nguvu zake
angezielekeza zaidi kwenye kukushauri na si kuibua yale ya utajiri wako
na mambo mengine.
Niliona ni busara hayo ya utajiri, pengine angeyaibua kabla au hata
baada ya sakata hili kupita kuliko kuliibua katika kipindi ambacho wewe
unatupa silaha zako katika kupambana na madawa ya kulevya. Ongeza nguvu
zaidi kaka, tuko nyuma yako.
Wewe umefanya, wengi wao wametutoa kwenye hoja ya msingi na kutupeleka kwenye hoja binafsi. Wanataka kutulisha mambo binafsi,
tusahau tatizo la msingi. Nikwambie tu mkuu wangu wa mkoa, usikate
tamaa, songa mbele. Pale ambapo unaona kunatolewa ushauri wa msingi
kuhusu vita hii, ni vyema ukauchukua na kuufanyia kazi.
Tunakubaliana kwamba katika kusaka suluhu ya jambo, si rahisi kusikiliza
kila mtu lakini kwa kuwa nawe ni kiongozi, hakika unao upeo wa kutosha
wa kung’amua mambo.
Tangu sakata hili limeanza, nimejaribu kufuatilia, wapo watu wengi sana
ambao wamekuwa wakishauri mambo ya msingi ambayo hata mimi naamini
ukiyasikiliza, bado yataongeza tija. Mfano ni lile suala la
kuwashughulikia kimyakimya, linaweza likatoa majibu chanya pia.
Kaka, una jeshi la polisi ambalo lipo chini yako, endelea kulimulika
nalo kwani maneno ya kwamba wao ndiyo sehemu kubwa ya tatizo yanasemwa
sana huku mtaani. Ni lazima uwe na askari juu ya askari. Wachungazane
wenyewe kwa wenyewe, usimuamini mtu mmoja. Tuwe na askari waaminifu,
watakaoweza kweli kutokomeza vijiwe vyote vya mitaani ambavyo
vinajulikana hata kwa watoto wadogo kwamba sehemu fulani kunauzwa unga.
Doria zifanyike mara kwa mara, wenyeviti wa mitaa kweli washiriki
kikamilifu katika vita hii maana wao wanawajua watu wao.
Lengo letu ni moja, sidhani kama unaweza kukataa kupokea ushauri ambao
nao una lengo la kujenga. Tunaamini kwa gia yako ya awali, unaweza pia
kubadili gia ya pili kama hiyo ya kimyakimya na mambo yakaenda vizuri.
Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa na nikutakie kila la kheri katika
mambo haya mazito ambayo umeyaanzisha.s
Mimi kama kijana mwenzio, nakuombea kwa Mungu, akupe ulinzi wake na
uweze kutekeleza vyema wajibu wako hapa duniani kwa nafasi ambayo Mungu
amekupa. Mimi ni ndugu yenu;
Erick Evarist
Tags
BIASHARA HARAMU
