Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama
hicho siku ya kesho tarehe 5 mwezi wa pili kitakuwa kikitimiza miaka 40
toka kimezaliwa, kimefanya mabadiliko katika kusherehekea siku hiyo kwa
kufanya shughuli mbalimbali za kijamii
Akiongea na EATV Humphrey Polepole amesema toka chama hicho kimeanzishwa
kimekuwa ni chama cha wananchama na chama ambacho kinashughulika na
masuala ya watu watu pamoja na matatizo yao, hivyo mwaka huu wameamua
kushurehekea siku hiyo kwa namna tofauti kwani hawatukuwa na sherehe
kama desturi yao bali watasherehekea kwa kushiriki shuguli za kijamii.
"Maadhimisho ya mwaka huu yatakuwa tofauti kidesturi kama ambavyo
yamefanyika hapo mwanzoni hivyo hatutakuwa na sherehe kama ilivyodesturi
ya mikutano mikubwa ya hadhara , kwa maana ya uzinduzi na kilele
isipokuwa mwaka huu tutafanya shughuli za maadhimisho ya CCM kwa namna
kuu mbili, moja ni kwa kushiriki shughuli za kijamii, shughuli ambazo
moja kwa moja zinagusa maisha ya watu wetu, jambo la pili ni mikutano ya
ndani na hapa wanachama wote wa CCM watashiriki mikutano ya ndani
kuanzia mikoa, ngazi ya wilaya, ngazi za majimbo, ngazi za kata na ngazi
za matawi kwa kushirikisha mashina yetu kote nchini Tanzania.
Mbali na hilo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
amesema kuwa maadhimisho ya miaka 40 ya CCM kwa mwaka huu yatafanyika
kwa mwaka mzima huu wa 2017.
Ikumbukwe kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa tarehe 5 Februari,
1977 kutokana na kuvunjwa kwa vyama vya Tanganyika African National
Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).
Tags
SIASA
