CHAMA cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha inadaiwa kimewafukuza uanachama
baadhi ya vigogo wake akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya
Arusha, Wilfred Soileli.
Wanachama hao wanatuhumiwa kukisaliti chama hicho kabla na baada ya
uchaguzi mkuu wakidaiwa kuwa wafuasi watiifu kwa Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa.
Wengine waliotimuliwa ni Mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa kutoka jimbo
la Arumeru Magharibi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC ) na
mfanyabiashara maarufu wa madini ya vito, Mathias Manga na Julius
Mungure wa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Wakati vigogo hao mkoani Arusha ikielezwa wamevuliwa uanachama wiki
iliyopita, Kamati ndogo ya Maadili ya CCM iliyokutana Dodoma iliwahoji
wanachama wake ambao wanadaiwa kukisaliti chama hicho.
Hao ni Profesa Juma Kapuya, Nazir Karamagi na Ally Sumaye ambao wote
wanadaiwa kukisaliti chama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Wana CCM hao waliohojiwa na kamati hiyo iliyoongozwa na Naibu Katibu
Mkuu Bara, Rodrick Mpogolo, ambaye gazeti hili lilipomtafuta kwa simu,
haikupokewa.
Taarifa zilizosambaa jijini hapa jana jioni zilidai uamuzi wa kuwafukuza
uanachama viongozi hao ulifanyika katika kikao cha Halmashauri Kuu ya
Mkoa wa Arusha kilichofanyika Jumamosi chini ya Mwenyekiti wa chama wa
mkoa huo, Lekule Laizer.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walisema kuwa Soileli na Manga
walituhumiwa kushirikiana kutoa siri na mikakati ya chama na kuipeleka
kwa viongozi wa Ukawa hasa Lowassa ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya
Rais.
“Hawa walionywa mara nyingi waache tabia ya kushirikiana na wapinzani
hasa Lowassa lakini Manga aliwahi kusema yuko tayari kuchukuliwa hatua
lakini asingeacha urafiki wake na Lowassa kwani siasa siyo uadui,”
alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho ambaye hakutata kutwa jina .
Tags
SIASA
