BAADA ya kupata dhamana ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi,
mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amelazwa tena kwenye Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Uhusiano wa Taasisi
hiyo jana, Anna Nkinda, Manji alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni
ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata dhamana dhidi ya kesi ya kutumia
dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili.
“Ni kweli Manji yupo hapa, aliletwa jana jioni (juzi) kwa matibabu
ambapo hadi leo (jana) ninavyoongea na wewe bado yupo hapa amelazwa
anaendelea na matibabu kama kawaida,” alisema Anna.
Hii ni mara ya pili kwa Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, kulazwa kwenye taasisi hiyo.
Mara ya kwanza ilikuwa ni Februari 12, mwaka huu alipolazwa hapo
akitokea katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alipokuwa
ameshikiliwa tangu Februari tisa akifanyiwa mahojiano.
Mfanyabiashara huyo alifika mwenyewe kwenye kituo hicho cha polisi
kutokana na wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, aliyetaja majina 65 ya watu aliodai wanajihusisha na biashara
ya dawa za kulevya.
Mbali na Manji, baadhi ya watu wengine waliotajwa na Makonda na kutakiwa
kufika kituoni hapo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat
Gwajima, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan ambao tayari
wamehojiwa polisi huku Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, akiwa bado
hajahojiwa licha ya kutajwa kwenye orodha hiyo.
Juzi Alhamisi, Manji alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
ambapo shauri lake lilisikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha.
Karani wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi, alimsomea mshtakiwa shtaka lake
ambapo alidai kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga
Sea View jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya
heroin.
Mtuhumiwa huyo alikana shtaka hilo na Mkurugenzi wa Mashtaka Msaidizi
(ADPP), Osward Tibabyekomya, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Upande wa mawakili wa utetezi ambao ni Alex Mgongolwa na Hudson
Ndusyepo, waliiomba Mahakama kumpa mshtakiwa dhamana kwa sababu ya
mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.
Hakimu Mkeha alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kutakiwa
kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na mdhamini mmoja wa
kuaminika ambapo Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa,
alimdhamini Manji, ambaye aliachiwa kwa dhamana hadi Machi 16.
Mara baada ya kupata dhamana, Manji aliondoka mahakamani hapo saa 9:40 akiwa kwenye gari yenye namba T670 BBX aina ya Hummer.
Tags
AFYA
