Wakati Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akigoma kula
hadi afikishwe mahakamani, wakili wake amepeleka maombi Mahakama Kuu
kuomba apewe dhamana baada ya polisi kuendelea kumshikilia kwa siku ya
tatu.
Wakili wa mbunge huyo, Peter Kibatala alisema mteja wake amefikia hatua
hiyo, baada ya Jeshi la Polisi linalomshikilia kumnyima dhamana bila
sababu.
“Hakuna sababu za msingi za kumnyima dhamana na tangu jana Lissu hajala
na amesema hatakula hadi afikishwe mahakamani,” alisema Kibatala na
kuongeza:
“Kosa analodaiwa kulifanya lilifanyika Januari 4 na hadi Februari 6 ni
mwezi, kama ni muda wa kuchunguza kosa hata hati ya mashtaka ingekuwa
tayari,” alisema Kibatala.
Alisema mteja wao (Lissu) analalamikia kuanzia ukamatwaji wake ulipoanza, alipokamatwa eneo la Bunge bila Spika kuwa na taarifa.
Kibatala alisema polisi waliokwenda kumkamata aliwatambua njiani na alikamatwa bila kuwapo kibali cha kukamata (arrest warrant).
Tags
HABARI KITAIFA
