Video Queen mwenye umbo ‘matata’ Bongo, Agnes Gerald ‘Masogange’,
amesoteshwa rumande na Jeshi la Polisi kufuatia kuendelea kumshikilia
katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam ‘Central’ kwa msala wa
madawa ya kulevya huku ndugu zake nao wakisota kwenye Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakisubiri apandishwe kizimbani bila mafanikio.
Februari 16, mwaka huu, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Simon Siro, lilithibitisha kumshikilia
mrembo huyo kwa mahojiano na vipimo juu ya tuhuma za kujihusisha na
utumiaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya huku likiahidi kumfikisha
mahakamani jana lakini likagonga mwamba.
Mapema jana, Risasi Jumamosi liliweka kambi mahakamani hapo likimsubiria
Masogange endapo atafikishwa na kupandishwa kizimbani kusomewa
mashitaka yake lakini hadi mawio, mrembo huyo hakufikishwa kwa madai ya
kutokamilika kwa upelelezi wa mashitaka yake.
Ndugu, jamaa na marafiki wa Masogange walijitokeza mahakamani tangu
asubuhi wakisubiria kama ndugu yao huyo atafikishwa mahakamani hapo
lakini hakuweza kufikishwa hivyo wakajikuta wakikata tamaa baada ya
kusota kwa muda mrefu hivyo kuondoka eneo hilo kwa huzuni na
kulengwalengwa na machozi.
Wakiwa kwenye banda la kusubiria, ndugu hao wa Masogange, muda mwingi
walisikika wakinung’unika kutokana na ndugu yao kukawizwa kufikishwa
mahali hapo kiasi cha wengine kuamua kwenda Central kuulizia kama
uwezekano wa kumleta utakuwepo.
Baadhi ya waliokwenda Central waliulizia kwa askali waliokuwepo kituoni
hapo na kujibiwa kuwa hataweza kufikishwa mahakamani jana kufuatia
majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali kukawia kufika polisi.
Baada ya hali kuwa hivyo, waliporudi Kisutu walikusanyana pamoja na
kuamua kuondoka mahakamani hapo huku wakilalama kuwa, ni kwa nini kama
polisi walifahamu wazi kwamba jana hawatamfikisha, wangewaambia ili
waendelee na shughuli zao.
“Hatujapendezwa kabisa na hali hii, maana kama walijua hawataweza
kumfikisha mahakamani leo (jana) hapakuwa na sababu ya kutuficha, maana
tungewaona wema kama wangesema tukaendelea na shughuli zetu.
“Hebu ona sasa hawajamleta na leo (jana) ni Ijumaa, kama siyo usumbufu
ni nini? Kutomleta maana yake si watamuweka hadi Jumatatu?,” walisikika
wakilalama baadhi ya ndugu hao.
Hadi Risasi Jumamosi linaondoka mahakamani hapo majira ya saa 10:00
jioni, Masogange alikuwa hajafikishwa kwa madai ya kutokamilika kwa
baadhi ya nyaraka za upelelezi wa kesi yake hiyo.
Tags
BIASHARA HARAMU
