WATU 20 wamekamatwa kwa msaada wa mbwa wa polisi mkoani hapa katika wiki
moja iliyopita, wakituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Watu hao walikamatwa baada ya Jeshi la Polisi kuanza kutumia mbwa
maalumu ili kusaka watuhumiwa wa madawa hayo, kwenye mabasi yanayopita
barabara kuu zinazoingia na kutoka mkoani Singida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Debora Magiligimba alisema njia hiyo
imesaidia kukamata watuhumiwa 20 ambao walikutwa na zaidi ya misokoto
7,000 ya bangi, 'unga' aina ya heroine na mirungi. Alisema kuwa zoezi
hilo litakuwa endelevu ili kukabiliana na wauzaji na watumiaji wa madawa
ya kulevya.
Kamanda Debora alisema wauzaji na watumiaji wamekuwa wakibuni njia mpya
kila siku kwa ajili ya kufanikisha "shughuli zao haramu".
Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imepata msukumo mpya tangu Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataje watu 65 waliotakiwa kuisaidia
polisi kuhusu biashara ya mihadarati wiki mbili zilizopita.
Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na viongozi wa dini,
wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya polisi 12
na wasanii kadhaa ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi,
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.
Vita hiyo ikaongezwa nguvu na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest
Manguvita ambaye naye aliamuru katika taarifa Makamanda wa mikoa yote
nchini waongeze nguvu.
Tangu hapo, zaidi ya watu 500 wamekamatwa katika mikoa mbalimbali nchini
wakihusishwa kwa namna moja au nyingine na biashara ya dawa za kulevya.
Katika matukio yote hayo ya ukamataji, hata hivyo, makamanda wa polisi
wa mikoa walielezea kukamata watuhumiwa bila ya kuhusisha mbwa waliopewa
mafunzo maalumu ya kugundua mihadarati.
Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Masauni
alikabidhiwa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser mbwa
maalumu wa kubaini madawa ya kulevya na pembe za ndovu mwaka jana, tukio
lililofanyika kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
ZOEZI ZURI
Abiria wa mabasi yaliyofanyiwa upekuzi kwa kutumia mbwa wa polisi na
kuzungumza na Nipashe, walieleza kufurahishwa na zoezi hilo kwa madai
kuwa litaondoa uwezekano wa kusambazwa ovyo kwa madawa hayo.
"Zoezi hili ni zuri sana, naomba liendelee ili kupiga vita uuzaji na
matumizi yake," alisema, Keneth Paul, abiria raia wa Marekani,
aliyesafiri na moja ya basi kutoka Arusha kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa.
"Mimi nilikuwa mtumiaji sana, lakini niliachana nayo na sasa nahubiri
injili. Awali akizungumza zaidi, Kamanda Debora alisema mtuhumiwa mmoja
aliyekamatwa na kete moja ya heroine, baada ya upelelezi alibainika kuwa
ni mtumiaji, lakini anaendelea na mahojiano zaidi ili kubaini
alikoinunua.
Alisema baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watapandishwa kizimbani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kamanda huyo wa polisi wa mkoa aliwataka wakazi wa mkoa wa Singida
kuendelea kushirikiana na jeshi lake ili kuunga mkono jitihada za
serikali ya awamu ya tano katika kutokomeza madawa ya kulevya nchini.
Rais wa tano, John Magufuli ameshaagiza vita hiyo isiache mtu yeyote.
“Hakuna mtu maarufu, mwanasiasa, waziri au kiongozi yeyote au mtoto wa
fulani, askari ambaye anajihusisha na dawa za kulenya aachwe, hata awe
mke wangu Janeth... kamata wote weka ndani,” alisema Rais Magufuli
mwanzoni mwa mwezi.
Aidha, Rais Magufuli pia ameshamteua Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia
na Kupambana na Dawa za Kulevya na kuweka msimamo wa Serikali yake juu
ya zaidi ya Watanzania 1,000 waliofungwa au kuhukumiwa kunyongwa katika
magereza mbalimbali duniani.
Rais Magufuli amesema serikali haitajishughulisha na Watanzania
waliokamatwa ughaibuni na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na kujihusisha
na biashara ya dawa za kulevya.
Tags
BIASHARA HARAMU
