Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli,
amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri
Mhe. Abdel Fattah El-Sisi ambaye amekubali nchi hiyo kuja kujenga
viwanda vya dawa nchini.
Katika mazungumzo hayo ambayo ni kando ya Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi
Wanachama wa Umoja wa Afrika uliomalizika jana Mjini Addis Ababa Nchini
Ethiopia viongozi hao wamezungumzia namna nchi hizo zitakavyoshirikiana
katika nyanja mbalimbali zikiwemo afya, kilimo, mifugo na viwanda.
Pamoja na kukubali mwaliko wa Rais Magufuli wa kufanya ziara rasmi
nchini Tanzania, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi pia amekubali ombi la
kuwaleta wataalamu na wawekezaji wa Misri nchini Tanzania ili wajenge
viwanda vya kuzalisha dawa na vifaa tiba vya binadamu, kuinua teknolojia
ya kilimo cha umwagiliaji, kuwekeza katika viwanda vya nyama na viwanda
vingine ambavyo nchi hiyo imepiga hatua kubwa.
“Mhe. Rais El-Sisi nakupongeza sana kwa juhudi zako za kuijenga Misri na
nitafurahi sana kuona biashara ya Tanzania na Misri inaongezeka
maradufu kwa manufaa ya pande zote mbili” amesisitiza Mhe. Dkt Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli pia amekutana na amekutana na Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambapo viongozi hao
wamezungumzia miradi mbalimbali ya ushirikiano na fursa za biashara
ambazo Tanzania na Uganda zinaweza kuzitumia kujiongezea mapato. Mhe.
Rais Museven amekubali kufanya ziara nchini Tanzania katika siku za
karibuni.
Tags
AFYA
