Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kwa kosa la
kupatikana na dawa za kulevya yanayodhaniwa kuwa heroine kiasi cha
pinchi 240 na ndonga mbili.
Taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa leo, imedai kuwa mtu huyo
aliyejulikana kwa jina la Kassim Hemed Kesi mwenye umri wa miaka 43,
amekamatwa majira ya saa 6 usiku wa kuamkia leo katika mtaa wa
Kanyerere kata ya Butimba wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza
Taarifa hiyo imedai kuwa mtu huyo ni mfanyabiashara wa spear za magari katika mtaa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kuwa awali
polisi walipata taarifa za mtuhumiwa huyo kuwa anajihusisha na biashara
ya madawa ya kulevya, hivyo askari walikuwa wakiendelea na upelelezi
pamoja na uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo.
Aidha wakati askari wakiendelea na upelelezi dhidi ya tuhuma za
mfanyabiashara huyo, jana tarehe 09.02.2017, polisi walipokea taarifa
kutoka kwa raia wema kwamba mtuhumiwa huyo ameingiza mzigo mkubwa wa
madawa ya kulevya kutoka Dar es Salaam na ameanza kuusambaza mtaani.
Tukio lilivyokuwa
Askari walianza kufanya ufuatiliaji wa haraka kuhusiana na taarifa hizo,
ndipo ilipofika majira ya saa sita usiku askari walifika hadi nyumbani
anapoishi mtuhumiwa na kuizingira nyumba yake yote na kumuona kupitia
dirisha akiendelea kufunga madawa hayo kwenye vikete vidogovidogo
maarufu kama pichi.
Wakati askari wanataka kuingia ndani ya nyumba mtuhumiwa alishtuka na
kukimbiza mzigo huo wa madawa ya kulevya chooni ili kupoteza ushahidi.
Aidha askari waliona kitendo kile kupitia dirishani na baadhi YA askari
waliingia ndani na kufanikiwa kukuta pinchi 240 zikiwa chooni lakini
bado hazikuwa zimetumbukia shimoni na kufanikiwa kuzitoa kwenye tundu la
choo.
Msangi amesema wakati huohuo askari wengine waliokuwa nje walikwenda
kuvunja bomba linalopitisha uchafu/choo linalokwenda kwenye shimo na
kuweka kizuizi hapo na kufanikiwa kupata ndonga 2 za dawa za kulevya
huku nyingine zikibebwa na maji .
Polisi wanaendelea na mahojiano na mtuhumiwa ili kuweza kubaini mtandao
wa watu aliokuwa akijihusisha nao katika biashara hiyo ya madawa ya
kulevya.
Tags
BIASHARA HARAMU