MBUNGE wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, ameiomba serikali kuhakikisha
inawalipa fidia wakazi wa Mloganzila ambao waliacha maeneo yao na
kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili (Muhas).
Akiuliza swali kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Mnyika alisema baadhi ya wakazi wa eneo hilo walilipwa lakini miongoni
mwao walipata kiasi ambacho hakilingani na maeneo yao, hivyo kuonekana
kupunjwa.
Aidha, Mnyika alitaka kufahamu kwa jinsi gani serikali inashughulikia
madai ya mapunjo ya fidia ya maendelezo kwa wakazi hao waliotakiwa
kuondoka kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Muhas.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Angelina Mabula, alisema ahadi
ya kuwalipa fidia ya kihisani yaani mkono wa heri iliyotolewa na
serikali Mei 20, mwaka juzi, itafanyika baada ya kupatikana fedha.
Mabula alisema malipo hayo hayajafanyika kwa muda kutokana na ukosefu wa
fedha kwenye bajeti, lakini pale zitakapopatikana hakuna atakayeshindwa
kulipwa.
Alisema tayari serikali ilishalipa Sh. 8,067,904,700 kwa ajili ya fidia
ya maendelezo ya ardhi kwa wananchi 1,919 katika kipindi cha 2008 mpaka
2010.
Aidha, alisema 2011 serikali ilitenga Sh. 1,610,374,700 kwa ajili ya
fidia ya wananchi 619 waliosalia katika malipo hayo ya fidia, wakiwa
wamewekeza ndani ya shamba mali ya serikali.
Hata hivyo, Mabula alisema mpaka sasa serikali haidaiwi mapunjo ya fidia kwa kuwa fidia ilikwishalipwa kwa mujibu wa sheria.A
Tags
Bunge
