JUMUIYA na Taasisi za Kiislamu nchini imevitaka vyombo vya kisheria na
uchunguzi kuacha kupuuza kauli zilizotolewa na wabunge zilizomtuhumu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumiliki mali zisizoendana
na kipato chake halali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
Msemaji wa Jumuiya hiyo Sheikh Rajabu Katimba, alisema wakati wa mkutano
wa Bunge lililopita baadhi ya wabunge walimtuhumu Makonda hivyo tuhuma
hizo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria.
Alisema vyombo vyenye mamlaka ya uchunguzi vinapaswa kufanya uhakiki wa
mali za Makonda ili kuondoa shaka katika umiliki wa mali aliyonayo na
uhalali wa misaada ya kifedha zinazotolewa kwake na taasisi rafiki.
Sheikh Katimba alisema kifungu cha (11) cha sheria ya maadili ya
viongozi wa umma inamtaka kiongozi kutaja hadharani mali zake ikiwemo
zawadi anazopewa.
Hivi karibuni, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) wakati
akichangia taarifa za Kamati ya Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
alisema Makonda amenunua jengo ‘(Apartment ) lenye thamani ya shilingi
mil 600 jijini Dar es Salaam.
Selesini aliliambia Bunge kuwa Makonda amempa gari mkewe aina ya
Mercedez Benzi lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani ambazo ni sawa
na Sh milioni 550.
Mbali na Selesini, Mbunge mwingine aliyemtuhumu Makonda kujilimbikizia
mali ni Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) ambaye naye
wakati akizungumza bungeni alihoji ni wapi Makonda alipata fedha za
kusafiri kwenye ndege daraja la juu kwenda Marekani.
Wakati huo huo, Sheikh Katimba alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inaweza kwenda vibaya iwapo itasimamiwa na wanasiasa.
Alisema ili kuepuka hilo vyombo vya dola vyenye mamlaka ya kisheria vinapaswa kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
Sheikh Katimba alisema taasisi za kiislamu zinaunga mkono jitihada
zinazofanywa na Serikali kupambana na biashara hiyo na kusisitiza kuwa
vyombo vyenye mamlaka kuisimamia kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na
Kupambana Dawa za Kulevya nchini ya mwaka 2014.
‘’Hatuoni ni kwa mantiki ipi watumiaji wengine washitakiwe kwa kutumia
dawa na wengine waachiwe huku zitumike na fedha za kuwatibia nje ya
nchi.
‘’Wasanii kama Rehema Chalamila, maarufu kwa jina la Ray C’ msanii TID
nao pia walipaswa kushitakiwa kama walivyofanywa wengine na vilevile
watumiaji walioko mitaani na kwenye vituo vya daladala wote wasombwe
wakapimwe na kisha washitakiwe.
“Pamoja na nia ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuongoza
na kuendesha vita hiyo lakini vita isimamiwe na vyombo vyenye weledi na
si wateule wa kisiasa au wanasiasa,’’ alisema.
Aidha, alizungumza kesi za ugaidi inawakabili baadhi ya viongozi wa dini
kwa kueleza kuwa haitakuwa na tija wala heshima iwapo viongozi hao
wataendelea kushikiliwa gerezani.
“Ni kweli serikali inatutaka tuiunge mkono kwenye vita hiyo nasi tuko
tayari lakini ni vuziri jitihada hii ikawa kwa watu wote, tunaiona
serikali inashindwa kutenda haki kwa viongozi wa dini yetu na ni kesi
gani isiyokwisha? inatia aibu masheikh kufungwa bila hatia miaka mitatu
ni sawa na kufungwa bila hatia,’’ alisema Sheikh Katimba.
Tags
HABARI ZA DINI
