WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaja mambo matano
makubwa, ikiwemo dawa za kulevya akisema wizara yake haina mjadala na
suala hilo kwani linagusa maisha ya Watanzania wote.
Nchemba alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
Ikulu Dar es Salaam baada ya kushuhudia viongozi mbalimbali wakiapishwa
na Rais John Magufuli.
Walioapishwa ni pamoja na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna
Makakala na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za
Kulevya, Rogers Sianga.
Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Omar Yusuph Mzee, Balozi
wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine na Balozi wa Tanzania nchini
Uganda, Grace Mgovano.
Waziri Mwigulu alitaja mambo mengine ni kupambana na ugaidi, ujangili wa rasimali za nchi, uhalifu wa kutumia silaha na ubakaji.
Alisema wamejipanga kukabiliana mambo hayo kutokana na ukweli kuwa
yamekuwa yakiongezeka kila kukicha hali ambayo inahatarisha amani ya
nchi.
Mwigulu alisema wizara yake kwa sasa imekamilika kila idara hivyo ni
wakati mwafaka wa kuhakikisha mapambano yote yanayohusika na mambo hayo
matano yanafanikiwa.
Alisema dawa za kulevya ni janga linalohitaji ushirikiano wa kada zote
hivyo wao wapo tayari kuhakikisha vita hiyo inakabiliwa kwa njia yoyote.
Waziri huyo alisema kwa siku za karibuni kumekuwepo na matukio ya
ubakaji na ujangili hasa nyara za Serikali akisema waanamini kwa pamoja
wataweza kupambana na wahusika.
“Tumejipanga kwa mambo makubwa matano ambayo ni dawa za kulevya,
ujangili, ubakaji, uhalifu wa kutumia silaha na ugaidi ambapo vyote kwa
pamoja vinashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu,” alisema.
Alitoa mwito kwa Watanzania kutoa ushirikiano wa mapambano mbalimbali ambayo yanafanywa na Serikali ili kudumisha amani ya nchi.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani imekuwa katika
mkakati wa kupambana na matukio mbalimbali ya uhalifu ambapo kwa siku za
karibuni mapambano hayo yameonekana kushika kasi hususan kwenye dawa za
kulevya ambayo yalianzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda.
Tags
BIASHARA HARAMU
