Serikali imepata kodi ya Sh466.4 kutokana na mauzo ya Sh9.3 bilioni ya
madini ya Tanzanite kupitia mnada uliofanyika mjini Arusha.
Akizungumza katika mnada huo, Mkurugenzi wa Uthaminishaji wa Almasi na
Vito Wizara ya Nishati na Madini (Tansolt), Archard Karugendo amesema
katika mauzo hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imepata Sh27.9
milioni.
Karugendo amesema katika mnada huo wa pili kufanyika nchini, Kampuni ya
TanzaniteOne inayomilikiwa kwa ubia kati ya Sky Associate na Stamico,
ndiyo iliongoza kwa kuuza madini na kupata Sh8.8 bilioni.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendela amesema licha ya madini hayo kuwa
ni ya Taifa, ni muhimu wakazi wa Wilaya ya Simanjiro waone matunda yake.
Bendera amesema ni aibu Tanzanite inatoka Simanjiro, lakini wilaya hiyo
ndiyo ya mwisho kwa elimu mkoani Manyara na kuwapo kwa shida kubwa ya
maji, huduma za afya na Mererani inaongoza kwa maambukizi ya HIV ambayo
yamefikia asilimia 18.
Wakizungumza baada ya mnada huo, wakurugenzi wa TanzaniteOne, Faisal
Shabhai na Hussein Gonga wameeleza kuridhishwa na kuahidi kuendelea
kushirikiana na wadau kuhakikisha wanauza madini katika minada nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe
amesema wizara hiyo, itaendelea kuwezesha minada ili kuhakikisha
wanunuzi wakubwa wa madini wanafika nchini kununua madini katika masoko
yanayotambulika kisheria.
Tags
UCHUMI / BIASHARA
