MAREKANI ilikuwa inasumbuka kuhusu mrithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere kama Rais wa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
1985, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) nani
angemrithi Mwalimu Nyerere lilikuwa ni suala ambalo liliumiza vichwa vya
taifa hilo tajiri duniani.
Kwa kawaida, CIA imekuwa na utaratibu wa kuweka hadharani baadhi ya siri
kuhusu ujasusi wake katika mataifa mbalimbali duniani; lakini baada ya
kipindi fulani kupita.
Safari hii, CIA imeweka hadharani siri za namna ilivyofuatilia matukio
mbalimbali katika siasa za kitaifa za Tanzania; hususani mwelekeo wake
endapo Nyerere angeondoka madarakani au angeendelea.
Kwa kawaida, ripoti hizo za CIA huwa zina ukweli ingawa wakati mwingine
–hasa kwa taarifa hizi mpya za Tanzania, kuna maeneo ambako ubashiri
wao unakuwa si wa kweli na upungufu mwingine katika usahihi wa majina ya
wahusika.
Musoma Group
Taarifa hizi mpya za kijasusi, zinaonyesha kwamba kuelekea mwaka 1985
ambako Uchaguzi Mkuu ulikuwa umepangwa kufanyika, kulikuwa na hali tete
kuhusu mwelekeo wa taifa.
Kwanza, nchi ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi baada ya kumalizika
kwa Vita ya Kagera na ilikuwa haieleweki kama Mwalimu ataendelea na
urais au atamwachia mtu mwingine.
Ripoti hiyo ya kikachero ya CIA; shirika kubwa zaidi la ujasusi duniani,
ilibainisha kwamba kulikuwa na kundi lililojiita Musoma Group
lililoanzishwa kwa minajili ya kumbembeleza Mwalimu asiachie madaraka.
“Kundi hili lilikuwa na watu watatu mashuhuri ambao ushawishi na nguvu
yao ya kiutawala ilitegemea sana kuendelea kuwapo kwa Mwalimu Nyerere
madarakani.
“Watu hao walikuwa ni Joseph Butiku aliyekuwa Katibu wa Mwalimu,
Timothy Apiyo aliyekuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri na Jenerali David
Musuguri aliyekuwa Mkuu wa Majeshi.
“Hawa walianzisha kundi hili kwa lengo la kumshawishi Mwalimu asiachie
urais. Wao walikuwa wakimshawishi aendelee kwa sababu nguvu yao
ilimtegemea zaidi yeye,” inadai sehemu ya ripoti hiyo.
Wahafidhina Vs Mrengo wa Kati
Ripoti hiyo ya aina yake, inadai pia kuhusu kuwapo kwa makundi mawili
kinzani ndani ya serikali katika siku za mwisho za urais wa Mwalimu.
Kulikuwa na kundi la wanasiasa wenye mrengo wa kihafidhina walioamini
kwamba Tanzania inaweza kuendelea kwa kufuata sera zake zilezile
ilizokuwa nazo tangu Uhuru.
CIA inadai kwamba kundi hili liliongozwa na Profesa Kighoma Ali Malima
(marehemu) na lilikuwa linaundwa na viongozi kama vile aliyekuwa Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Charles Nyirabu, Msaidizi Binafsi wa
Mwalimu, Joan Wickens (raia wa Uingereza), Butiku na Kingunge Ngombale
Mwiru.
Kundi hili lilikuwa katika misuguano ya mara kwa mara na kundi la
waumini wa siasa za mrengo wa kiliberali wanaodaiwa kuongozwa na Cleopa
Msuya.
Ripoti hiyo inawataja wanachama maarufu wa kundi hili kuwa ni aliyekuwa
Katibu Mkuu Hazina, Fulgence Kazaura, aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki ya
NBC, Amon Nsekela, George Mbowe na Profesa Simon Mbilinyi.
Wakati wahafidhina walikuwa wakishikilia msimamo ambao uliendana na ule
wa Mwalimu, waliberali walitaka serikali ikubaliane na mapendekezo ya
mashirika ya fedha ya kimataifa na wahisani ili ikopesheke na kuweza
kufufua uchumi wake.
Dk. Salim na Ali Hassan Mwinyi
Nyaraka hizo za siri za CIA ambazo safari hii zimetolewa kwa amri ya
Mahakama moja ya Marekani, kwa undani pia zimeeleza kuhusu wanasiasa
wawili waliokuwa wakipewa nafasi ya kumrithi Nyerere endapo angekuwa
tayari kuachia ngazi.
Wanasiasa waliotajwa ni aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Waziri
Mkuu wakati huo, 1984, Dk. Salim Ahmed Salim.
Ripoti za CIA zinadai kwamba Nyerere angependa mmoja wa wawili hao awe
mrithi wake – Mwinyi akifanikiwa kupata nafasi hiyo hatimaye, lakini
wote walikuwa na masuala ambayo yalimpa Mwalimu shaka.
“ Salim alikuwa na uzoefu mkubwa katika medani ya kimataifa kwani
alitoka kuhudumu nje ya nchi. Tatizo lake ni kwamba hakuwa na mizizi
katika siasa za Tanzania kwani kufikia wakati huo alikuwa ametumia
maisha yake yote ya utumishi nje ya nchi.
“Kwa kumpitisha Salim, Nyerere hakuwa na uhakika kama watu ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyombo vya ulinzi na usalama wangemkubalia
–hasa ukizingatia nchi ilikuwa ikipita katika kipindi kigumu kiuchumi.
“Kwa upande mwingine, Mwinyi naye hakuwa na ushawishi mkubwa Tanzania
Bara lakini kwa Mwalimu alionekana kama ni mtu ambaye asingeweza kufanya
mabadiliko makubwa katika sera zilizokuwapo wakati huo,” inaeleza
ripoti hiyo ya CIA kuhusu Tanzania ya mwaka 1984.
Pamoja na maelezo haya ya CIA, mahojiano yaliyowahi kufanywa huko nyuma
na gazeti hili kuhusu mchakato wa kumpata mrithi wa Nyerere ndani ya CCM
yana maelezo tofauti kuhusu suala hilo.
Kwa mfano, wanahistoria kama Joseph Mihangwa ambaye pia ni mwanasafu wa
Raia Mwema, amewahi kueleza kwa kina kuhusu nini hasa kilitokea wakati.
Kwa maelezo yake, Nyerere alikuwa amemuandaa Edward Moringe Sokoine kuwa
mrithi wake lakini kifo cha Waziri Mkuu wake huyo kilivuruga mpango
wake huo.
Mihangwa pia anadai kwamba Salim ndiye aliyekuwa chaguo la Mwalimu
lakini fitna na ubaguzi katika siasa za Zanzibar ndizo hatimaye
zilizompa ushindi Mwinyi.
“Kulikuwa na makundi mawili kuelekea uchaguzi wa kumpata mrithi wa
Nyerere. Kundi la kwanza ni la vijana waliokuwa wakifahamika kama Young
Turks waliokuwa wakimuunga mkono Salim.
“Kundi la pili lilikuwa linaundwa na wahafidhina wa Mapinduzi ya
Zanzibar ambao walimhusisha Salim na chama cha Hizbu kilichohusishwa na
mauaji ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Abeid
Amani Karume.
“Kundi hili la pili lilifanya kampeni kali dhidi ya Salim huku
likiungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa NEC kutoka Tanzania Bara. Hivi
ndivyo namna Mwinyi alivyoshinda,” aliandika Mihangwa.
Mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Getrude Mongella, anayetajwa
kuwa katika kundi hili la wahafidhina, aliwahi kuzungumza na gazeti
hili pia na kusema ingawa Mwalimu alijulikana kumpenda Salim, hakutumia
mamlaka yake kuzuia walio wengi kumpitisha Mwinyi.
Ugumu wa Mwalimu Nyerere
Katika mambo ambayo nyaraka hizo za CIA zimeeleza kwa kina ni namna
Marekani ilivyokuwa ikihofia ushawishi wa Nyerere katika siasa za
Tanzania na dunia kwa ujumla.
Kwanza, CIA iliripoti kwa mamlaka za juu kuwa Nyerere, hata katika
kipindi hicho cha matatizo nyumbani kwake, alikuwa na heshima kubwa
katika medani ya kimataifa, kiasi kwamba mwaka huo wa 1984, alikuwa na
nafasi kubwa ya kuchaguliwa na wenzake kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Nchi
Huru za Afrika (OAU).
CIA ilimtaja pia Nyerere kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa
katika Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) na medani ya
kimataifa kwa ujumla.
Nyaraka hizi zimeonyesha namna Nyerere alivyokuwa mwiba kwa Wamarekani;
ripoti ikidai alikuwa akiishambulia Marekani kila alipopata fursa,
ingawa pia imekiri kuwa Baba wa Taifa alikuwa mwiba pia kwa Urusi ya
zamani.
Ripoti hiyo imetoa mfano wa mashambulizi makali ya maneno aliyoyatoa
Mwalimu kwa Urusi, baada ya kuwa imeivamia kijeshi nchi ya Afghanistan.
Tags
HISTORIA
