Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeahidi kujadili deni
linalodaiwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linalofikia Sh300.6
bilioni.
Tanesco inadaiwa deni hilo na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutokana na mradi wa bomba dogo la gesi.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka amesema wameipokea ripoti ya TPDC
na kutokana na umuhimu wake, kamati hiyo itakaa kujadili na kutoa
uamuzi.
“Kama unavyoona, shirika hili limepewa jukumu kubwa la kuhakikisha
linasambaza gesi kwa Watanzania ili kuwezesha utunzaji wa mazingira. Ni
lazima tuwasaidie waweze kupata fedha za maendeleo,” alisema.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka amesema deni
hilo linaendelea kulipwa kidogokidogo na kwamba hata wiki iliyopita
walipunguza.
Akizungumza katika mkutano wa TPDC na PAC, Mwenyekiti wa bodi wa shirika
hilo, Profesa Sufian Bukurura amesema pia wanaiomba kamati hiyo
kuwasaidia ili wapate fedha za maendeleo ambazo Serikali iliahidi
kuzitoa kama njia ya kukuza mtaji.
“Tungezipata hizo fedha tungeweza kulipa deni la Sh100 bilioni tunalodaiwa na taasisi mbalimbali,” amesema.
Tags
HABARI KITAIFA
