BANDA MEDIA BLOG

WAHARIRI TUMIENI KALAMU ZENU KUELIMISHA UMMA FAIDA ZA MTO NILE.


maafi1Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya wahariri wa vyombo vya habari yaliyoandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji leo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji wa Wizara hiyo, Mhandisi Sylvester Matemu na kushoto ni Mratibu wa Kanda (NELSAP), Elicad Nyabeeya.
maafi2Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari nchini wakisikiliza kwa makini mafunzo kuhusu maana, faida na malengo ya Bonde la mto Nile yaliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

………………………………………………………………
   Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Wahariri wa vyombo vya habari wameaswa kutumia taaluma yao kuhabarisha umma kuhusu maana, faida na malengo ya Bonde la mto Nile kwa wananchi wa ukanda wa mto huo ili waweze kutumia fursa waliyonayo katika kujiletea maendeleo.
Mafunzo hayo yametolewa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Sylvester Matemu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana pamoja na Mratibu wa Kanda (NELSAP), Elicad Nyabeeya.
Akiongea na wahariri hao, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Sylvester Matemu amesema kuwa maadhimisho ya siku ya Nile kufanyika nchini ni tukio la kihistoria kwasababu linatokea kwa nchi moja kila baada miaka 10 hivyo ni muhimu kwa wahariri wa vyombo vya habari kuwa na ufahamu juu ya jambo hilo ili wakahabarishe umma.
“Lengo la Siku ya Nile ni kukuza uelewa kwa watu wote kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zote wanachama, masuala yanayotekelezwa na faida inayopatikana kutokana na matumizi bora ya rasilimali za Bonde la Mto huo, hivyo, vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuhabarisha umma ndio sababu iliyotufanya tuwape mafunzo hayo,” alisema Mhandisi Matemu.
Aliongeza kuwa tukio hilo ni kubwa kitaifa kwani litahudhuriwa na watu zaidi ya 600 wakiwemo Mawaziri wa nchi wanachama kutoka kwenye nchi husika na maadhimisho hayo yanatarajiwa kufunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia shughuli za wanachama wa Bonde la Mto Nile (NBI), Innocent Ntabana amesema kuwa azma ya kusimamia na kuendeleza rasilimali za Bonde la Mto Nile limepewa kipaumbele na nchi zote zilizozungukwa na mto huo, jambo hilo ndilo limesababisha kuanzishwa kwa Sekretarieti ya NBI mwaka 1999 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa NBI ina jukumu la kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji za Bonde la Mto Nile kwa niaba ya nchi wanachama zipatazo 10 ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Sudan, Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na  Misri.
Kwa upande wake Mratibu wa Kanda (NELSAP), Elicad Nyabeeya amesema kuwa mto huo una manufaa makubwa kwa nchi wanachama kwani muunganiko wa nchi hizo umeleta mawasiliano mazuri ambayo yanapelekea kuinua uchumi wa nchi hizo pia kwa upande mwingine uwepo wa ushirikiano huo umesaidia nchi wanachama kufahamu tamaduni za watu tofauti tofauti.
“Nchi ya Tanzania inafaidika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na NBI kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa bwawa la Bisrawi na usanifu wa bwawa la Borenga, mkoani Mara”
“Pia nchi hii itanufaika na miradi ya maji na nishati ya umeme, pamoja na miradi mingine mingi ambayo NBI inaendelea kuitekeleza kama vile ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo na umwagiliaji katika mabonde ya mito Kagera na Ngono, mkoani Kagera,” alisema Nyabeeya.
Maadhimisho ya Siku ya Nile yanatarajiwa kufanyika Februari, 22 mwaka huu kuanzia saa 02:30 Asubuhi, yataanza kwa maandamano yatakayoongozwa na Bendi ya Polisi kuanzia viwanja vya Mnazi Mmoja hadi Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo maonesho pamoja na ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo vitafanyika.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG