Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli
Jumatatu hii amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein
Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu,Jaffar Haniu imesema:
Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yao wamezungumza mambo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtakia heri Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia leo
kuwa siku yake ya kuzaliwa
Kwa upande wake Rais Dkt. Ali Mohamed Shein amesema anamshukuru Rais
Dkt.Magufuli kwa kumtakia heri katika siku yake muhimu ya kuzaliwa na
hivyo wamekutana kubadilishana mawazo katika kuhakikisha wanajenga nchi
na kusonga mbele.
“Siku ya kuzaliwa ni siku ya furaha lazima ikumbukwe lazima
isherehekewe, mimi siku yangu ya kuzaliwa sisherehekei sana lakini huwa
nafurahi sana na leo nimefurahi sana” amesema Dkt. Shein.
Dkt.Shein amesema ametumia siku yake ya kuzaliwa kumtembelea Rais
Dkt.Magufuli ili waweze kubadilishana mawazo kwani wana kazi kubwa ya
kujenga nchi.
