Bilionea maarufu nchini Marekani aliyefahamika zaidi kwa kutoa pesa
kuwasaidia watu wasiojiweza sehemu mbalimbali za dunuia, David
Rockefeller amefariki dunia akiwa usingizini nyumbani kwake Poncantico
Hills, New York akiwa na umri wa miaka 101.
Kupitia Taasisi yake ya The Rockefeller Foundation alifanikiwa
kufadhili ujenzi wa majengo marefu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) mwanzoni mwa miaka ya 1970.
Rockefeller alikuwa mtoto wa mwisho kwenye familia watoto watano wa
kiume wa John D Rockefeller Jr. Ndiye aliyekuwa mjukuu wa mwanzilishi wa
kampuni ya Standard Oil John D Rockefeller.
Mzee huyo ndiye aliyekuwa anasimamia mali na biashara za familia hiyo,
pamoja na miradi yake ya kusaidia jamii, ingawa hakuwahi kutafuta
wadhifa wowote wa kisiasa, kaka zake wawili walihudumu serikali.
Nelson Rockefeller alifanya kazi kama gavana wa New York na kwa muda
kama Makamu wa Rais wa Marekani huku Winthrop Rockefeller naye alikuwa
gavana wa Arkansas.
David Rockefeller alihitimu kutoka chuo kikuu cha Harvard mwaka 1936 na
kutunukiwa Shahada ya Uzamifu Katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha
Chicago mwaka 1940.
Alitumikia Jeshi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na baadaye
akafanya kazi katika benki ya Chase Bank, ambayo baadaye ilikuwa benki
ya JP Morgan Chase.
Bw Rockefeller alimiliki kazi za sanaa za thamani ya $500m (£404m).
Alipokuwa anasherehekea kutimiza miaka 100 mwaka 2015, alitoa ardhi ya ekari 1,000 kwa mbuga ya taifa katika jimbo la Maine.
Juhudi zake za kusaidia jamii zilimfanya kutunukiwa Nishani ya Uhuru ya Rais mwaka 1998.
Alikuwa na watoto wanne – David Jr, Richard, Abby, Neva, Margaret na
Eileen. Mkewe Margaret (jina lake la kuzaliwa McGrath) alifariki 1996.
