Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam,
Inspekta Prisca Komba amewaonya madereva bodaboda kuwa na mahusiano ya
kimapenzi na mabinti wa shule na badala yake wawe mstari wa mbele
kulinda na kuwasaidia kutimiza malengo yao
Akizungumza leo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwenye
kipindi cha East Africa Breakfast cha EA Radio, Inspekta Komba amesema
katika dawati lake la jinsia kesi nyingi anazopata ni za madereva
kuwapatia mimba wanafunzi na kisha kuwatelekeza kitu ambacho kinamuumiza
zaidi ni pale binti anakuwa ammeachishwa shule na mwenye mimba anakuwa
kakimbia
"Huwa naumia sana nikiwa napokea kesi za aina hii. Unajua hawa bodaboda
siyo vijana wabaya lakini niwaambie kwamba, kama umempenda binti wa watu
fuata njia sahihi za kumpata, siyo tena kumharibia masomo yake na mtoto
umtelekeze maana hata wakati mwingine huwa hawasemi kweli wanapoishi,
boda boda waacheni wanafunzi wasome.
Aidha Bi. Komba ameongeza kuwa licha ya kuhitaji mabinti walindwe
kuepukana na mimba za utotoni lakini pia ameiomba jamii nzima
kuhakikisha mtoto wa kike anathaminiwa kwa kupatiwa taulo za kujisitiri
wakati wa hedhi hasa kwa wale wanafunzi wanaotoka katika mazingira
magumu.
"Hili jambo hebu tusiachiwe wanawake tu kwa sababu lipo katika miili
yetu. Kama mimi mwanamke mume wangu hatonithamini kwa kuninunulia vifaa
vya kusitiria nikitumia vifaa vichafu nikipata magonjwa naye
nitamuambukiza, kwa kuangalia hivyo hili jambo ni letu sote." Amesema
Komba.
Tags
ELIMU
