
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi, Willbrod Slaa amesema anajitathmini
kwa kile kilichomfanya aondoke hapa nchini na familia yake kama hakipo
aweze kurejea nyumbani.
Dkt. Slaa aliamua kuweka pembeni masuala ya siasa baada ya kutofautiana
na chama chake juu ya masharti ya kumpokea aliyekuwa mgombea wa Urais wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Amesema kuwa kwa sasa amemaliza masomo yake na baada ya kutafakari na kujitathmini atarejea nyumbani muda wowote.
“Ni kweli nimemaliza masomo yangu, bado napima mazingira yaliyonifanya
niondoke na familia yangu, baada ya hapo nitaangalia uwezekano wa
kurejea nyumbani,”amesema Dkt. Slaa.
Aidha, kuhusu mwenendo mzima wa Serikali ya awamu ya Tano, amesema kuwa
hakuna nchi hata moja ulimwenguni ambayo Rais wake atakubarika kwa
asilimia mia moja, hivyo Rais Magufuli ameonyesha msimamo wa kusimamia
kile anachokiamini
Hata hivyo, ameongeza kuwa kama wapinzani hawatakuja na ajenda makini na
mkakati unaoweza kuwasaidia wananchi hapo walipo, basi upinzani unaweza
kufutika mwaka 2020.
“Kama nilivyorejea mara kadhaa, upinzani makini utaingia Ikulu kwa
ajenda mbadala. Ajenda makini yenye kuwalenga wananchi moja kwa moja
katika kuwatoa kwenye kero zao mbalimbali.
“Hadi sasa ninachoona ni ‘kurukia’ kauli za JPM, lakini kauli si ajenda
na hatupeani maksi kwa kuzungumzia usahihi wa lugha. Wako wanaotazama
usahihi wa lugha na mahali pa kutazama usahihi huo. Kimsingi hayo ni
masuala ya darasani au kwenye uandishi wa vitabu.
“Aidha kumtuhumu JPM kukiuka Katiba na sheria nayo haina tija. Wote
wanaomtuhumu wanajua kuwa wakiambiwa waonyeshe kifungu mahususi
alichokiuka yeye mwenyewe katika utendaji wake hawana majibu ya
kuridhisha.
“Hivyo mimi sijaona mwenendo wa JPM unaosaidia kuingiza upinzani Ikulu.
Isitoshe kama hawatakuja na ajenda makini na mkakati ulioandaliwa
unaowatoa wananchi hapa walipo kwenda kwenye raha, upinzani unaweza
kufutika kabla ya 2020,”alisema Dk. Slaa.
Tags
Dr Slaa