MENEJA wa msanii wa Bongo Fleva, Bill Nass na County Boy anayefahamika
kama Ahmed Salum ‘Petit Man’, ameongelea fedheha na hasara iliyomkuta
alipokumbwa na kashfa ya kuhusishwa na dawa za kulevya na kujikuta
akiswekwa lupango.
Katika mazungumzo juzi, Petit Man, alisema kitendo cha kukaa mahabusu
kwa wiki moja kimempotezea fedha nyingi ambazo alikuwa amepanga kuingiza
kwa wiki ile ili kuwafikisha hatua nyingine wasanii wake wanaomtegemea
yeye kwa asilimia kubwa.
“Naumia sana nikizungumzia suala hili kwa sababu naona ni moja ya vitu
ambavyo vilitaka kunitia umasikini, pesa (fedha) niliyoipoteza wiki ile
ilikuwa ya kunitoa sehemu moja kwenda nyingine, ilikuwa nyingi na
nilitarajia kufanya mengi sana,” alisema Petit Man.
Aliongeza kuwa mahabusu si sehemu nzuri kwani amejifunza mengi sana na
amekumbana na watu tofauti ambao wengine ameweza kuwasaidia na wengine
imeshindikana.
Akizungumzia kipigo alichodaiwa kupigwa, Petit Man, alisema kutangaziwa
kupigwa ilikuwa kama fedheha kwake akikiri kwamba alipata misukosuko ya
kawaida na si kipigo kama ilivyovumishwa.
“Nadhani Kamanda Sirro (Simon) ni askari mkubwa na msomi, sidhani kama
anaweza kutoa adhabu isiyostahili na inayokiuka haki za binaadamu na
mimi nilipata adhabu yangu kama mtuhumiwa na yote hiyo ilikuwa ni kupata
ukweli na si mimi pekee, nadhani wengi walipata adhabu ili waseme, sasa
huo uvumi mwingine mimi siutambui na huwa sipendi kuongelea naona kama
umeniletea fedheha kwenye jamii, kila mtu anatafsiri yake,” alisema
Petit Man.
Aliongeza: “Mimi sina rekodi mbaya, nina imani hii adhabu kabla ya
kuisha nitapewa ruhusa ya kufanya mambo yangu kwa uhuru, hakuna
asiyenijua mimi ni mtu wa aina gani, napenda sana kushirikiana na watu
wa aina zote na kumsaidia mtu pale ninapoweza.”
Akizungumzia sakata la aliyekuwa swahiba wake wa muda mrefu, Wema
Sepetu, kuhama chama, alisema kila mtu ana mawazo yake na utashi wake
hivyo kama ameamua kufanya hivyo, basi inabidi wao wawe wasikilizaji
kwani Miss Tanzania 2016 huyo ana wazazi wake na kwamba hayo ni
mapendekezo ya mtu.
Hata hivyo, aliweka wazi akisema: “Mimi na Wema bado ni familia moja
japokuwa kila mtu ana kampuni yake, niliamua kutoka kwenda kwenye
kampuni ili kujitafutia kipato na nitaendelea kushirikiana naye kwa kazi
ambazo tulikuwa tukifanya.”
Pia alizungumzia ndoa yake na mkewe, Esma Kandili ‘Esma Platinumz’
ambaye ni dada wa msanii nguli wa Bongo Fleva, Nassib Abdul ‘Diamond’,
akisema anaamini ndiye mwanamke aliyechaguliwa na Mungu na katu
hatafikiria kwenda kwingine.
“Nina amini Esma ndiye mwanamke niliyechaguliwa na Mungu, tulijaribu
kutengena ila ilishindikana na kujikuta kila mmoja akimhitaji mwenziye
na sasa ndoa yetu imerudi, ifahamike ndiye aliyenipa heshima ya kuitwa
baba baada ya kufanikiwa kupata mtoto aitwaye Taraj,” alisema Petiti
Man.
Tags
BIASHARA HARAMU
