Wakati
nchi ya Tanzania ikiadhimisha wiki ya maji,imeelezwa kuwa wanawake wengi
wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamekuwa wakitumia muda mwingi
kutafuta maji hivyo kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo
kikamilifu.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia muda wao
mwingi kutafuta maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu
na Maswa mkoa wa Simiyu kabla na baada ya Uhuru wa Tanganyika mpaka sasa
hali inayowafanya kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume.
Wakizungumza na waandishi wa habari
waliotembelea wilayani humo wananchi wa vijiji vya Nyenze na
Ng’wang’holo kata ya Mwadui Lohumbo wilayani humo walisema maji ni
changamoto kubwa inayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi kwani
wanatumia muda mwingi kutafuta maji.
Walisema licha ya kuishi karibu na mgodi
wa almasi wa Williamson wanalazimika kutembea umbali takribani kilomita
tano kufuata maji katika mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Kishapu na
wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.
Akielezea changamoto hiyo,mkazi wa
kijiji cha Nyenze Agnes Daudi alisema akina mama ndiyo waathirika
wakubwa kwani wamekuwa wakitumia muda wao mwingi kutafuta maji na mara
nyingi huamka kila siku majira ya saa 11 alfajiri kwenda katika mto huo
na kurudi nyumbani saa 4 asubuhi.
“Licha ya kutumia muda mwingi kufuata
maji,hayo maji yenyewe ya mto Tungu siyo salama kwani yanatumiwa pia na
wanyama kama fisi na watu wengi kijijini huwa hawachemshi maji
wanakunywa hivyo hivyo”,alieleza Daudi.
Aliongeza kuwa kutokana na changamoto
hiyo,wanawake wapo hatarini kushambuliwa na wanyama aina ya fisi ambao
wamekuwa wakikutana nao mara kwa usiku wanapofuata maji mtoni.
Naye Anastazia Lutamla walisema maji
yamesababisha migogoro katika ndoa kwani wanaume wamekuwa wakiwatuhumu
wake zao kuwa wanachelewa kurudi nyumbani kwa kisingizio cha maji.
“Wanawake wanakumbana na changamoto
nyingi njiani ikiwemo kubakwa,wasukuma ni waoga wengi wamekuwa hawasemi
vitendo wanavyofanyiwa wakiamini kuwa ni fedheha mbele ya jamii”,aliongeza Lutamla.
Grace Maige mkazi wa kijiji cha
Ng’wang’holo aliiomba serikali na mgodi wa almasi wa Williason,Karspian
na El-Hilal vilivyo karibu na vijiji hivyo kuimarisha ujirani mwema kwa
kuwapatia huduma ya maji wananchi kwani wamekuwa wakitaabika kwa muda
mrefu sasa.
Naye Tungu Magega ambaye jina lake
linatokana na mto Tungu ambapo alizaliwa wakati mama yake akichota maji
katika mto huo mwaka 1949 alisema vijiji vinavyozunguka mgodi wa
Williamson vilipaswa hudumiwa na mgodi huo hata kwa kuwachimbia visima
tu.
“Nilizaliwa mwaka 1949,nipo katika
kijiji hiki cha Nyenze tatizo la maji ni changamoto kabla na baada ya
uhuru,tunaomba serikali itusaidie kuondoa tatizo hili,kama mgodi
umeshindwa kutuhudumia,basi tunaomba hata maji kutoka ziwa Victoria yaje
kijijini kwetu”,alieleza Magega.
Afisa Mtendaji wa kata ya Mwadui Lohumbo
James Limbe alisema ni kweli kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya
maji na kwamba jitihada wanazofanya sasa ni kuboresha visima vilivyopo
katika baadhi ya vitongoji vilivyoharibika wakati wakisubiri maji kutoka
ziwa Victoria kufika katika kijiji hicho.
Limbe alisema wanawake katika kata hiyo
wanapoteza muda mwingi kwa badala ya kufanya shughuli zingine za
maendeleo kwa kufuata maji katika mto Tungu ambayo hata hivyo siyo
salama kwa maisha ya binadamu.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga
Talaba alisema suala la ukosefu wa maji lipo kwa wilaya hiyo ni kame
lakini serikali inafanya jitihada za kuwapatia maji wananchi ambapo
tayari bomba la maji kutoka Ziwa Victoria yameshafika katika mji wa
Mhunze wilayani humo.
“Siyo kweli kuwa wananchi wote
wanatumia maji ya mto Tungu,wengine wana visima,mabwawa,hivi sasa mradi
wa maji kutoka ziwa Victoria unaendelea Kishapu,ukikamilika tutapata
maji, tatizo ni upatikanaji wa pesa”,alieleza Nyabaganga.
“Kadri tutakavyopata pesa tutapeleka
maji vijijini,tumeanza na mji wa Mhunze,kila kijiji palipopita bomba
tumeweka toleo la maji,tenki letu lipo mbioni kukamilika,bomba tayari
limeshatandazwa”,aliongeza Talaba.
Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani
Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa
mto Tungu unaotenganisha wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu na Kishapu mkoa
wa Shinyanga,mto huo ni tegemeo kubwa la wananchi wa wilaya ya Kishapu
kutokana na uhaba wa maji.
Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akichota maji ya kunywa baada ya kufukua mchanga pembezoni mwa mto Tungu
Watoto wa kike wakipeleka mifugo yao kunywa maji katika mto Tungu huku mwananchi akiendelea kufua nguo
Mkazi wa kata ya Mwadui Lohumbo wilayani Kishapu akitoka mto Tungu kuchota maji ya kunywa
Haya ni mashimo yaliyofukuliwa pembezoni
mwa mto Tungu ambapo maji hujichuja kutoka kwenye mto na kuingia kwenye
mashimo hayo na wananchi kuchota maji hayo kwa ajili ya kunywa
Shimo lililofukuliwa pembezoni mwa mto Tungu
Mchungaji wa mbuzi,ng’ombe akipeleka mifugo yake mto Tungu
Wananchi wakifua nguo katika mto Tungu
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Tags
KERO YA MAJI



