Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa
kuwa Serikali haitatoa chakula cha msaada kwa watakaopatwa na njaa
ilihali wanaweza kuzalisha chakula katika maeneo yao.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo jana katika ziara yake mkoani Pwani,
wakati akizungumza na wananchi wa Somanga, Nangurukuru na Mchinga Moja,
ikiwa ni ziara yake katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara.
Amepokea kero za wananchi katika maeneo hayo na kufanya kazi kwa bidii ikiwemo kuzalisha mazao ya chakula cha kutosha
"Najua mmezoea kusikia maneno mazuri mazuri kuwa hakuna atakayekufa kwa
njaa, sasa mimi nasema usipofanya kazi, usipolima mazao na kupata
chakula wakati mvua inanyesha Serikali haitatoa chakula cha bure kwa
wenye njaa, ni lazima tufanye kazi, sasa hivi mvua zinanyesha limeni
mazao ya chakula" amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Ikwiriri na kupokea kero
zao ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji katika Mji huo kuhakikisha mradi
wa maji uliojengwa na kukamilika tangu mwaka 2015 kwa gharama ya
Shilingi Bilioni 5, unaanza kutoka maji kabla ya mwisho wa Mwezi huu na
pia amepiga marufuku utozaji wa ushuru kwa wafanyabiashara wadogowadogo
wa mazao.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Lindi
kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji iliyoanza kuibuka mkoani
humo na ameahidi kutoa Shilingi Milioni 20 kusaidia ujenzi wa Zahanati
ya Somanga.
Tags
HABARI KITAIFA
