Kamishna msaidizi, kanda ya ziwa; Joseph Shewiyo akisoma taarifa ya Utekelezaji ya kanda ya ziwa, mkoani Mwanza.
Naibu
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Angeline
Mabulla akikagua mfumo wa Kielekroniki wa ukadiriiaji ulipaji wa kodi ya
Ardhi wilaya ya Iringa Mkoani Iringa.
………………………………………………………………………….
Viwanja 60,808 vimepimwa na
bilioni 6 kukusanywa kama kodi ya pango la Ardhi mpaka kufikia mwezi
Februari 2017 mkoani Mwanza. Kamishna wa Ardhi msaidizi, Kanda ya Ziwa;
Joseph Shewiyo alieleza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Kanda ya
Ziwa.
Alieleza; katika mwaka huu wa
2016/17 mojawapo ya malengo maalum ya Kanda yamekuwa ni kufuatilia na
kuwezesha upimaji na umilikishaji milki 60,000. Utekelezaji wa jukumu
hili unajumuisha kupanga matumizi ya ardhi, kupima na kutoa milki.
Umilikishaji unafanyika baada ya kukamilishwa kwa malipo ya ada za milki
za viwanja ambavyo mamlaka za ardhi zimegawa kupitia Kamati za Kugawa
Ardhi au viwanja vilivyoandaliwa kwa utaratibu wa urasimishaji wa maeneo
ya wananchi. Hatahivyo hadi kufikia Februari, 2017, uhakiki umefanyika
wa viwanja vilivyopimwa, na kuonekana kufikia viwanja 60,808, ambapo
kati ya hivyo wamiliki 3,648 wamelipia na kupewa hati.
Aliendelea kusema katika
makusanyo ya maduhuli yatokanayo na ardhi; Hadi kufikia Februari, 2017,
karibu shilingi bilioni 6 zimekusanywa. Aidha lengo la makusanyo ni
shilingi bilioni 11. Mkakati umeandaliwa wa kuhakisha kuwa, kila mwenye
ardhi analipa deni. Vilevile wale wote watakaoshindwa kufanya malipo
watafikishwa Mahakamani na ardhi zao zitanadiwa kwa amri ya Mahakama
kulipia madeni yao.
Alisema; “Kwa Jiji la Mwanza na
Manispaa ya Ilemela tayari tumekamilisha orodha ya wadaiwa sugu zaidi ya
421 wanaodaiwa zaidi ya shilingi bilioni 2. Wadaiwa hawa watafikishwa
Mahakamani muda wowote kuanzia sasa, hawa ni baadhi tu ya wadaiwa na
uhakiki bado unaendelea”.
Aidha, kwa ujumla Majukumu
makubwa ya ofisi ya Kanda ni kuidhinisha kazi za ardhi ambazo awali
zilikuwa zinaidhinishwa Wizarani na kusimamia kazi zinazofanywa na
mamlaka za upangaji yaani Halmashauri za Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya
za utekelezaji wa Sheria za Ardhi na malengo ya Serikali.
Katika kutoa huduma za ardhi na
kujibu hoja za wananchi; Kamishna Shewiyo alisema; Hadi kufikia
Februari, 2017 wananchi 13,009 wamesikilizwa na kuhudumiwa. Jumla ya
barua 1,061 zimepokelewa na kujibiwa katika ofisi ya Kanda. (Hawa
hawajumuishi waliofika ofisi za Halmashauri). Aidha, mikutano 9 ya
hadhara iliitishwa na viongozi wa Wizara (Waziri na Naibu Waziri) katika
Halmashauri za Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela, Bukoba, Musoma,
Bunda, Magu, Maswa na Chato. Hoja za wananchi zilisikilizwa na kupokea
kero zipatazo 482. Kero hizi zinafanyiwa kazi na majibu yanatolewa kwa
wananchi husika.
Aidha, Kamishna Shewiyo alisema
Kanda imejipanga kuhakikisha kuwa malengo yanakamilika pamoja na
changamoto mbalimbali zilizopo. Kamishna Shewiyo, amewasihi wananchi
kuwa na ushirikiano katika kuwezesha na kurahisha utoaji wa huduma za
ardhi kwa kuwasiliana na viongozi wa Kanda pale ambapo wanapewa huduma
au majibu yasiyo ridhisha.
Hapo awali Kanda ya ziwa ilikuwa
inashughulikia mikoa mitano ambayo ni Geita, Kagera, Mara, Mwanza na
Simiyu ambayo kwa ujumla ina Halmashauri 37. Kwa sasa kanda ya ziwa
itakuwa inashughulikia mikoa mitatu tu, ambayo ni Mwanza, Geita na
Kagera. Na Makao makuu ya Kanda yataendelea kuwa Mwanza. Aidha, Mikoa
iliyoachwa ya Mara na Simiyu imejumuishwa kwenye Kanda nyingine mpya ya
Simiyu; pamoja na mkoa wa Shinyanga, ikiifanya kanda hiyo kuwa na mikoa
mitatu pia, na makao makuu yake yakiwa Simiyu.
Tags
HABARI KITAIFA