Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini ALAT Bwana Gulam Mukadam
amemsimamisha kazi Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Bw Abraham Shemoboyo
kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa shilingi milioni 150 za
ufadhili wa jumuiya hiyo mwaka 2015.
Akiongea katika ofisi za jumuiya hiyo Jijini Dar es salaam, Gulam
ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga amesema, benki ya
NMB ilitoa kiasi hicho cha pesa kwa jumuiya hiyo kwaajili ya ufadhili wa
Tuzo ya Meya (Mayor Awards) na kwamba Katibu huyo huyo hakuwasilisha
kiasi chote na badala yake aliwasilisha shilingi milioni 60 huku kiasi
cha shilingi milioni 90 kikiwa hakijulikani kilipo.
Mukadam amesema, uamuzi wa kumsimamisha uliamuliwa na kamati tendaji ya
ALAT Taifa na mkutano mkuu wa ALAT taifa, ambapo iliundwa tume ndogo
kuchunguza upotevu wa kiasi hicho cha pesa na kuamuliwa kuwa apishe
uchunguzi dhidi yake kwa upotevu wa pesa hizo.
Aidha Mstahiki Mukadam amesema, uchunguzi dhidi yake utafanywa na CAG na
kwamba pesa hizo hazikuwekwa kwenye akaunt ya ALAT na badala yake
zilihifadhiwa kwenye akaunti binafsi ijulikanayo kama 'Vision
Investment'.
Tags
HABARI KITAIFA
