MWANASIASA mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema hatua ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kuwaadhibu makada wake hivi karibuni ni mwendelezo wa
makosa yaliyoongozwa na kuratibiwa na viongozi wakuu watatu wa chama
hicho wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais takribani miaka miwili
iliyopita.
Kingunge mmoja wa waasisi wa CCM aliwataja viongozi hao ambao alisema
kimsingi ndio wanapaswa kubeba dhamana ya usaliti ndani ya chama hicho
kuwa ni Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti Bara,
Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
Kingunge aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili
yaliyofanyika wiki hii katika makazi yake yaliyoko eneo la Victoria,
Dar es Salaam.
Katika mahojiano hayo ambayo yalidumu kwa saa moja na dakika 22,
Kingunge ambaye amepata kufanya kazi na serikali za awamu zote nne,
alizungumzia demokrasia, haki, utendaji wa Serikali ya awamu ya tano na
hali ya siasa, ikiwamo uamuzi wa hivi karibuni uliochukuliwa na CCM.
Kuhusu yaliyotokea wiki iliyopita ndani ya CCM, ikiwa ni pamoja na
kuwaadhibu wanachama wake kwa makosa ya usaliti, Kingunge alisema si
mapya bali ni mwendelezo wa makosa yaliyotokea wakati wa mchakato wa
kumpata mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015.
Aliyataja makosa yenyewe kuwa ni yale ya ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kumpitisha mgombea wa urais.
Alisema uongozi wa CCM wa wakati huo chini ya uenyekiti wa Kikwete,
Makamu Mwenyekiti Bara, Mangula na Katibu Mkuu Kinana, kwa pamoja
walifanikiwa kushawishi Kamati Kuu (CC) kuvunja Katiba na kanuni za
chama hicho.
Kingunge ambaye hii si mara yake ya kwanza kueleza kile alichokiona ni
ukakasi wa mfumo uliotumika na vikao vya juu vya CCM kumpata mgombea wa
kiti cha urais, alihoji katika mazingira ya leo ya kuwashuku fulani ni
wasaliti wakati unajua kuna watu walikiuka taratibu na kanuni za chama,
ni nani anayepaswa kuitwa msaliti?
Kwa muktadha huo, alisema CC ilishindwa kufanya kazi yake kama
inavyoelekezwa na katiba na kanuni zake, hivyo ikajikuta imekataa
kuwasikiliza, kuwaona na kuwahoji wagombea 38 wa urais, badala yake
wakakubaliana na mapendekezo ya majina yaliyotoka kwa Kikwete.
“Huko kwenye NEC baada ya vurumai kubwa ndiko wakapatikana hao wagombea
watatu ambao walipelekwa kwenye mkutano mkuu na mwisho wake akapatikana
Bwana Magufuli,” alisema.
Kingunge alisema kuwa imekuwa kama alivyosema Mwalimu Nyerere, kwamba ukishakula nyama ya binadamu hutakoma, utaendelea tu.
KUFUKUZA WANACHAMA
Akizungumzia hatua ya CCM kuwafuta uanachama baadhi ya viongozi, kuwapa
onyo na kuwasamehe wengine kwa sababu ya kile kinachoitwa usaliti,
mwanasiasa huyo alisema anastaajabu adhabu hiyo kuwagusa baadhi wakati
msingi wake ni mchakato wa kumpata mgombea urais 2015.
“Kwa hawa waliohukumiwa, wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na
mchakato kumpata mgombea wa urais, sasa swali linakuja, hapo katika
mchakato wa kumpata mgombea urais, aliyesalitiwa ni nani? Ni CCM ndiyo
iliyosalitiwa ama kuna mgombea fulani maalumu ambaye ndiye
aliyesalitiwa?
“Kwa ninavyoijua Katiba ya CCM na kanuni zake, hadi wakati ule wa
kumtafuta mgombea, mazingira yalikuwa ya ushindani huria (huru),”
alisema.
Kwa mtazamo wake, alisema wagombea wote walifuata taratibu za kuchukua
fomu hadi kutafuta wadhamini na kuhoji hadi katika hatua hiyo nani ni
msaliti na alimsaliti nani?
“Kwa sababu huo ulikuwa ni utaratibu ndani ya CCM… wadhamini waliomuunga
mkono mmoja hawakuruhusiwa kwa mwingine. Sasa wadhamini waliomuunga
mkono ‘A’ ndio walikuwa wasaliti kwa sababu hawakuwaunga mkono wengine
waliobaki?” alihoji Kingunge.
Kwa mujibu wa Kingunge, vikao vya juu vya CCM wajumbe walikuwa na haki
ya kujadili sababu za baadhi ya wagombea kuwamo na wengine kutokuwamo.
“Sophia Simba alimsaliti nani, Madabida alimsaliti nani na katika ngazi
gani? Ndiyo maana nasema hili suala lote hili ni mwendelezo wa
yaliyotokea 2015, Agosti 10 kule Dodoma, pale ambapo uongozi wa chama,
kundi la watu watatu likiongozwa na Kikwete ndilo lilifanya CC na jopo
la wazee wastaafu washirikiane na wakubaliane kuvunja katiba na kanuni
na wao kuchukua jukumu la kuteua watu watano nje ya utaratibu uliowekwa
na chama,” alisema.
Alihoji wanachama waliofukuzwa wamemsaliti nani kwa sababu wakati wa
mchakato kila mwanachama alikuwa na mgombea wake anayemuunga mkono.
MAAMUZI YA KAMATI YA MAADILI
MTANZANIA Jumapili lilimkumbusha kwamba majina hayo yalipitishwa katika Kamati ya Maadili ya chama.
Lakini katika maelezo yake Kingunge alifafanua kwamba Kamati ya Maadili
wakati wa kipindi hicho ilikuwa ni kitengo ndani ya Ofisi ya Katibu
Mkuu, hivyo haitambuliwi ndani ya Katiba ya CCM.
Alisema kwa sasa anaona kuna jitihada za kutaka kuibadili Kamati ya Maadili kiwe kikao rasmi.
“Katika suala la maadili ndani ya chama, mkuu wa maadili ni NEC na
katika ngazi zote za chama kuanzia taifa hadi matawi,” alisema.
Kwa mujibu wa Kingunge, kuanzia mwaka 1982 wakati ulipoanzishwa mfumo mpya wa chama, ilikuwapo Tume ya Udhibiti na Nidhamu.
Alisema tume hiyo ilikuwa na hadhi ya idara ya chama, lakini baadaye
yakafanyika marekebisho, hivyo suala la maadili halikujumuishwa katika
hadhi ya idara ya chama na badala yake likawa ndani ya kitengo ambacho
kipo chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu.
“Kwa hiyo, Kamati ya Maadili haina majukumu ya kikatiba ya kuwa na kauli
juu ya nani awe au asiwe mgombea, lakini inaweza kuishauri CC na NEC na
kamati hiyo haiwezi kutoa ushauri wa kuvunja katiba na anayeshauriwa
ndiye mwamuzi,” alisema.
MADARAKA YA KIIMLA
Akiendelea kufafanua hoja hiyo, Kingunge alisema madaraka yanatakiwa kujengeka kwa misingi ya hoja na si misingi ya kiimla.
Alisema pamoja na kwamba yeye si mwanachama wa CCM kwa sasa, lakini ana
haki za kutoa maoni juu ya uamuzi huo kama raia wa Tanzania.
Kwamba kama raia wa nchi hii, anataka vyama vya siasa vilivyopo vijengeke katika misingi ya demokrasia.
“Hatuwezi kuwa na vyama feki feki tu, kwa hiyo inavyotokea kwamba chama
cha siasa hapa nchini kinafanya vitabia ivitakavyo bila kusimamia
misingi ya demokrasia, sisi kama raia tuna haki ya kukihoji na kama
kimekosea tutawaambia wamekosea na katika hili CCM imekosea,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba ameachana na CCM, lakini ana historia na chama
hicho. Alitanabaisha kuwa yeye ni miongoni mwa waasisi wa CCM na alikuwa
kwenye jopo la watu 20 waliounda kamati ya kuandaa rasimu ya katiba ya
chama hicho (1976-1977).
Alisema kuwa ndani ya CCM amehusika na utangulizi na yaliyomo katika katiba ya chama hicho.
“Watu waliomo CCM waelewe, ile katiba ni kitu kikubwa sana na tuliiunda
ili ibebe mema yote ya TANU na ASP, ibebe misingi iliyotuongoza kufanya
mambo makubwa sana katika TANU na ASP, misingi hiyo ni demokrasia, haki,
usawa na utu.
“Sasa wanaodai kwamba wanaongoza CCM wakifanya mambo ambayo hayafanani
na ile tuliyoiunda, mimi inanipa tabu na katika hilo siwezi kunyamaza
nitasema tu… naweza nikasema nyinyi CCM yenu mliyoiunda ni nyingine,
siyo yetu ya akina Kingunge na wenzake,” alisema.
CCM INAINGIA PAGUMU
Kingunge alisema CCM inajiingiza katika hali ngumu, kwa sababu ya baadhi
ya viongozi ndani ya chama hicho kujiaminisha kuwa wanajua kila kitu.
“Hii inatokana na jambo moja, lazima niliseme. Binadamu sisi tumepewa
vichwa na ndani ya vichwa kuna akili ambayo imepewa kazi ya kufikiri,
lakini hakuna binadamu anayejitosheleza katika masuala ya kufikiri, sasa
ukifika mahala kwamba baadhi ya binadamu wanajiaminisha kwamba wao
wanajua kila kitu, ndio chanzo cha matatizo,” alisema.
CCM HAITAKI MIJADALA
Kingunge alisema kwa yanayofanywa sasa ndani ya CCM, ni wazi inaonekana haitaki mijadala.
“Mkutano Mkuu wa Taifa ulifanyika kwa saa tatu, mkutano ambao ulikuwa
na jukumu la kujadili mabadiliko ya katiba… saa tatu umwekwisha kila
kitu… sasa nasema tunalo tatizo katika nchi hii, kwanza mijadala nje ya
chama haitakiwi, sasa hawa wenye nchi yao kwahiyo itakuwa ada yao ni
kupewa amri tu?
“Wanapewa amri na watawala na ada yao itakuwa ni kutii amri za watawala?
Hakuna kuhoji. masuala yanayotokea katika nchi yao, hawa raia hawana
haki ya kuyajadili,” alisema.
Akithibitisha kauli yake hiyo, Kingunge alitolea mfano jinsi wale wanaotangaza baa la njaa wanavyopewa adhabu.
NCHI IENDESHWE AU IONGOZWE?
Alisema nchi imefika mahali sio pazuri kwa sababu ya viongozi na alitoa mifano ya njia mbili za kufuatwa.
“Kuna njia mbili, ama nchi iendeshwe au nchi iongozwe, kama mnataka nchi
iongozwe maana lazima mkubali wananchi wenyewe watoe maoni yao halafu
mnakwenda, lakini mnataka kuiendesha nchi na mnajua matokeo ya nchi
kuiendesha,” alisema.
Aliongeza kwa kusema kuwa ni lazima kila Mtanzania, kuanzia viongozi, wote kujitahidi kuondoa munkari na hasira.
“Hamuwezi kuwa na nchi viongozi wanaonekana wana hasira tu na raia nao
wataonekana kuwa na hasira, tukifika hapo nchi haiendi. Nasema tuwe
watulivu sote, wakubwa kwa wadogo ili tuwe wanyenyekevu kwa sababu sisi
ni watu tu, ukiwa mkubwa ni mtu, ukiwa mdogo wewe ni mtu.
“Mkubwa mambo yake ya msingi anayoyafanya ni yale yale anayoyafanya mtu
mdogo, kwahiyo sisi wote ni watu ndiyo maana Katiba ya CCM inasema
binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa utu
wake,” alisema.
Aliongeza kwa kusema kama Watanzania wote wanataka kuijenga nchi, wanaweza kuijenga, lakini kama wanataka kuibomoa wataibomoa.
CCM IMECHOKA
Kingunge alikwenda mbali na kusema kwamba CCM si kwamba imeishiwa pumzi tu, bali imechoka.
Alisema mazingira hayo yanakifanya chama hicho kukosa nguvu ya kwenda mbele kwa sababu ndani yake kumekosekana umoja.
“Hakuna suala kubwa katika ‘organization’ (taasisi) yoyote kama umoja,
muundo wowote wa watu wanaotaka kufanya jambo kwanza kabisa ni umoja,
Mwalimu Nyerere alitufundisha wakati ameanzisha TANU na wenzake 17.
Alisema suala la kwanza ni umoja, Waafrika tuungane kumtoa mkoloni.
“Na katika harakati za kujenga umoja kunatokea vitu vingi, zinatokea
nguvu nyingine zinazotaka kuwaweka pembeni ili mtengane… uongozi
unatakiwa kuelewa masilahi ya chama ni nini… kuna kuelewa masilahi yako
na vikija vishawishi vya kujitenganisha na wenzako, unajiuliza kama
linafifisha harakati au linaendeleza, hivyo unajirudi na kuendelea na
mapambano,” alisema.
WALIFUKUZWA CCM
Katika hatua nyingine, Kingunge aliwatia moyo watu waliovuliwa uanachama wa CCM na wale waliopewa onyo.
Aliwataka wasibabaike kwa sababu kama bado wanaipenda CCM waombe warudishwe.
Lakini akasema: “Dunia si CCM, kwa sababu kabla yake kulikuwa na TANU. Kwani binadamu hawakuishi?”
