JESHI la Polisi limeanza uchunguzi mkali kuwatafuta waliohusika
kufanikisha mauaji ya kinyama ya Samira Masoud (34), ambaye ni mke wa
mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Samira aliuawa nyumbani kwake, eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam, na
kisha mwili wa marehemu kukutwa ukiwa kwenye chombo kikubwa cha kuwekea
maji cha namna ya beseni.
Akizungumza jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SACP Susan Kaganda, alisema mwili wa Samira ulikutwa
Jumanne ya wiki hii baada ya taarifa kupatikana kutoka kwa ndugu wa
marehemu, ambaye ni mke wa mwanajeshi wa JWTZ (jina linahifadhiwa).
Akisimulia zaidi, Kamanda Kaganda alisema kuwa Jumanne ya wiki hii,
majira ya saa 11:00 jioni, ndugu wa marehemu walifika katika kituo cha
polisi kutoa taarifa kuhusu marehemu ambaye ni dada yao.
Alisema ndugu hao waliwaeleza polisi kuwa, kwa muda mrefu walikuwa
hawana mawasiliano na dada yao, lakini siku hiyo (Jumanne), walipokea
ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi ya Samira.
Kamanda alisema ujumbe huo ulikuwa ukisomeka kuwa, “Nendeni mkachukue maiti ya ndugu yenu… itaozea ndani.”
Alisema baada ya kuona ujumbe huo, ndugu hao walikwenda nyumbani kwa
marehemu, lakini hawakuingia ndani baada ya kukuta gari lake lipo nje ya
uzio. Waliamua kwenda kutoa taarifa polisi.
Aidha, alisema baada ya taarifa hiyo, polisi kwa kushirikiana na ofisi
ya Serikali ya Mtaa wa Kibamba, walifika eneo hilo na kuvunja nyumba na
ndipo walipokuta mwili wa marehemu kwenye chombo cha maji huku ukiwa
umeharibika vibaya.
“Tumejaribu kila mara kuipiga simu ya marehemu ambayo ilitumika kutuma
ujumbe kwa ndugu wa marehemu, lakini imezimwa…mume wake ambaye ni
mwanajeshi wa JWTZ, ambaye alikuwa kwenye mafunzo ya kijeshi visiwani
Zanzibar, alikuja baada ya kupewa taarifa za kifo cha mke wake. Hivi
sasa bado hakuna anayeshikiliwa,” alisema Kamanda Kaganda.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili na kwamba, hivi sasa wanasubiri ripoti ya daktari ili kujua
kwa kina namna Samira alivyouawa.
Tags
JWTZ