Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba amewataka maafisa wa
jeshi hilo kutenda haki kutokana na baadhi yao kunyooshewa vidole kwa
kukiuka misingi ya kazi zao ikiwamo kujihusisha na rushwa.
Waziri Nchemba pia amelitaka jeshi hilo kuhakikisha linaendelea na
mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwamo vita dhidi ya matumizi ya
dawa za kulevya huku akiahidi dhamira ya serikali katika kuongeza
maslahi ya askari polisi nchini pamoja na miundombinu ya makazi yao.
Ametoa agizo hilo katika kikao cha kazi kilichoongozwa na mkuu wa jeshi
la polisi nchini IGP Ernest Mangu na kuhudhuriwa na maafisa waandamizi,
makamanda wa mikoa na wakuu wa vikosi vya polisi nchi nzima ambapo
pamoja na mambo mengine kinajadili mikakati ya kukabiliana na uhalifu
nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Waziri Nchemba amesema
serikali itaendeleza jitihada zake za kuwakomboa askari katika kuongeza
maslahi yao pamoja na kuboresha miundombinu ya askari
Kwa upande wake mkuu wa jeshi la polisi nchini IGP Ernest Mangu amesema
mapambano dhidi ya madawa ya kulevya imekuwa ni tatizo sugu nchini na
kuitaka jamii kutofumbia macho vitendo hivyo vya kihalifu.
Tags
Mwigulu Nchemba