Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa siku 14 kwa Shirika la
Visiwani Zanzibar (ZECO) kulipa deni lote la ankara za umeme wanalodaiwa
na endapo halitafanya hivyo basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa
ikiwa ni pamoja na kukatiwa umeme.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo
Dkt. Tito Mwinuka alipokuwa anaongea na waandishi wa habari Jijini Dar
es Salaam ambapo amesema hadi kufikia mwezi Januari mwaka 2017, Shirika
la Umeme Zanzibar (ZECO) lilikuwa linadaiwa zaidi ya shilingi bilioni
127.8.
“Shirika la umeme linashindwa kutekeleza majukumu yake mbalimbali kwa
wakati ikiwemo uendeshaji wa shirika, matengenezo ya miundombinu pamoja
na utekelezaji wa miradi, hayo yote yanasababishwa na malimbikizo ya
madeni kwa wadaiwa sugu hivyo tunatoa siku 14, wasipoweza kulipa
tutawakatia huduma ya umeme”. Alisema Dkt Mwinuka
Aidha mbali na ZECO, Tanesco imewataja wadaiwa sugu wengine ikihusisha
Wizara na Taasisi za serikali zikiwa zinadaiwa zaidi ya bilioni 52.5,
makampuni binafsi pamoja na wateja wadogo wanaodaiwa zaidi ya bilioni
94.9
Kwa upande mwingine Dkt. Mwinuka amesema shirika hilo linatarajia kuanza
oparesheni maalum ya kukusanya madeni hayo na matarajio yao ni kulipwa
kwa malikimbizo yote ili yalisaidie kujiendesha kiushandani na kwa
ufanisi mkubwa zaidi na kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali
zinazotegema nishati ya umeme nchini.
Hatua hii imekuja ikiwa ni takriban siku 4 tangu Rais Magufuli kuagiza
TANESCO kufuatilia madeni yote ikiwemo deni ambalo TANESCO inalidai
ZECO, na kuitaka kuwakatia umeme wote watakaoshindwa kulipa kwa wakati.
Tags
ZANZABAR
