Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewaomba wanachama wa CCM
wanaoanza mkutano mkuu wao maalumu kesho, kuweka mbele uzalendo badala
ya ushabiki wa kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema wanachama wa CCM wanapaswa
kuutumia mkutano huo kuisema Serikali yao kuhusu kupuuza mambo ya
msingi, ikiwamo malengo ya bajeti iliyopitishwa na Bunge.
Alisema imekuwa kawaida kwa Serikali kupuuza mambo ya msingi na kufanya
ambayo hayamo kwenye bajeti huku baadhi ya maeneo yakikosa huduma
muhimu.
Dk Mashinji alitoa mfano kuwa, mwaka wa bajeti wa 2016/17 unakaribia
kwisha, lakini kiuhalisia utekelezaji wake uko robo ya nne na haujafikia
asilimia 40.
Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema mbali na hayo, Serikali haitaki
kusimamiwa kikamilifu na inauyumbisha mhimili wa Bunge ambapo vikao vya
kamati za Bunge vimeshindwa kuanza kama ilivyopangwa awali kwa wiki
tatu, badala yake muda umepunguzwa hadi wiki mbili. Aliongeza kwamba
bajeti iliyopitishwa imekuwa haiheshimiwi na kuingiziwa matumizi ambayo
hayakuwemo ikiwamo Serikali kuhamia Dodoma, kujenga kiwanja cha ndege
Chato na Magereza ya Ukonga
Tags
CHADEMA
