MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi
yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe ya kutaka asikamatwe hadi kesi yake ya kikatiba
dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda itakapomalizika.
Maombi hayo yalitupwa kwa sababu kifungu cha sheria kilichotumika
kuyafungua si sahihi na kwamba hutumika pale ambapo sheria ziko kimya.
Uamuzi huo wa majaji umefikiwa kutokana na pingamizi la jamhuri
lililowasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Gabriel Malata kuiomba
kuyatupilia mbali maombi hayo kwani hayana msingi kisheria.
Katika hatua nyingine, mwanahabari nguli nchini Jenerali Ulimwengu,
ameungana na jopo la mawakili Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Malya
katika kumtetea Mbowe.
Mbowe amefungua kesi hiyo ya kikatiba namba 1, ya mwaka 2017 dhidi ya
wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Kesi hiyo itasikilizwa
tena Machi 8, mwaka huu.
Tags
SIASA
