NIMEKUKUMBUKA leo mama wa muigizaji Wema Isaac Sepetu. Habari za hapo
Sinza-Mori, familia yako haijambo? Vipi mnaendeleaje? Najua utashangaa
kwa nini leo nimekuandikia barua lakini usishtuke, huu ni utaratibu
wangu wa kila wiki.
Huwa nawaandikia watu mbalimbali mashuhuri kama wewe mama. Eeeh! Mwanao
amekufanya na wewe usikauke kwenye vyombo vya habari. Hongera yako.
Labda tu nikuibie siri kidogo mama, barua hii ni tofauti na zile
nyingine ambazo mara nyingi huwa zinasomwa na watu wawili; muandikaji na
muandikiwa.
Barua hii inasomwa na mamilioni ya Watanzania ambao watapata fursa ya kujipatia nakala tu ya gazeti hili kwa shilingi mia tano.
Hilo si dhumuni la kukuandikia barua hii. Ngoja nienda moja kwa moja
katika hoja. Mama nimekuandikia kwa lengo moja tu, kukuambia kwamba
hukupaswa kumfanyia vile muigizaji Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ katika
sakata lako na mwanao, hata kama ulikuwa una lengo la kumtumia kama
‘silaha’ kwenye vita unayoiendesha.
Mosi, kwa heshima uliyonayo kitendo tu cha kumrekodi (naamini upande wa
simu yako ndiyo ulirekodi, yaweza pia kuwa vinginevyo), kilikuwa si cha
kiungwana. Kitendo kile pengine kingefanywa na vijana kwa vijana, kidogo
kingeeleweka lakini si wewe kama mzazi.
Pili, kama alivyosema Steve, kwa wazo lako la kurekodi limesababisha pia
wewe usikike ukifanya masihara ambayo kama ni kweli umehusika
kuyasambaza, ukitafakari vizuri utaona jinsi gani yanakurudia wewe
mwenyewe.
Yanakudhalilisha maana umesikika ukizungumza mambo yasiyopendeza
kutamkwa na mtu mzima mbele ya hadhara. Kitendo cha wewe kuaminika
umemrekodi Steve, kimeleta matokeo ya wewe kuvujisha utani wa kijinga
usiopendeza kwa mama na mwanaye.
Steve amesikika akikutania kwamba anataka mzae mtoto, utani mbaya ambao
kwa namna moja au nyingine, haupendezi kusikika na mamilioni ya
Watanzania. Kwa anayewaza vizuri, hawezi kumrekodi mtu katika mambo ya
siri kama yale na kwa namna yoyote ile kuyarusha mitandaoni.
Niliposikiliza ile sauti, kwangu niliona ni kama matusi. Mama yangu,
jambo lile lingefanywa na vijana wenzake Wema, lingekuwa na picha yenye
ahueni lakini wewe kusikika unatoa lugha chafu kwa kijana kama utani, ni
aibu.
Jamii nzima itapata tabu sana kukuamini hata kama ulikuwa na lengo jema
katika jambo hilo au umevurugwa kiasi gani. Kama mama, hata kama
umekosewa, waswahili wanasema huwezi kumfukuza chizi akiwa mtupu na wewe
ukiwa mtupu.
Utajistahi kwanza ndipo umkimbize. Kwa namna yoyote, heshima yako
inapaswa kubaki palepale. Kama Steve alivyosema, hakutegemea ungeweza
kumrekodi kwani anakuheshimu kama mzazi wake. Steve alisema alizungumza
na wewe kirafiki kama mama na mwanaye.
Alizungumza na wewe akiamini huwezi kumsaliti au kumfanyia vitendo
vitakavyomhatarishia maisha yake ya baadaye kama ulivyofanya. Pamoja na
hayo yote, kama vile mlivyokuwa mnaitaka haki na mwanao, hamkupaswa
kuidai kwa kuvunja haki. Maana kwa
mujibu wa sheria ya makosa ya mtandao ni dhahiri itakugusa kwa namna
moja au nyingine. Yale ni mazungumzo binafsi, yametokaje kwenye mitandao
ya kijamii? Mwisho, nikushauri, wewe ni mzazi kuna mambo ambayo
unapaswa kuyazungumza mbele ya jamii mengine weka akiba. Si vyema ukawa
unatengeneza picha kwamba kila ukionekana, utamwaga povu kama ulivyosema
siku ile kwenye mkutano wa waandishi wa habari.
Naamini mama utakuwa umenielewa. Nimezungumza kiungwana, naomba nawe uwe
muungwana katika kila hatua unayopiga kwenye safari yenu na kila
unalolifanya, ni vyema kufikiri mara mbilimbili na kujua hatima ya jambo
unaloliamua.
Tags
SIASA
