Bado Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (36) anaendelea kutajwa
kwenye vinywa vya Watanzania wengi kufuatia madai ya kutumia vyeti
ambavyo vinasemekana si vya kwake, lakini Amani sasa limebaini mambo 6
yanayomponza bosi huyo.
Kwa takriban wiki ya tatu sasa, jina la Makonda limekuwa likiandikwa
kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kwa ishu hiyo ya vyeti ambapo,
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar, Joseph
Gwajima ndiye aliyeibua madai hayo mazito kiasi cha kuifanya jamii
kuyavalia njuga madai hayo.
ILIKUWA KWENYE IBADA YA JUMAPILI
Gwajima aliibua sintofahamu ya vyeti hivyo, Jumapili ya Februari 26,
mwaka huu, kwenye mahubiri ya ibada ya kanisani kwake, Ubungo ambapo
alisema kuwa, Makonda anatumia cheti cha kidato cha nne cha mtu
anayeitwa Paul Christian Muyenge wakati yeye alianza darasa la kwanza
mwaka 1988, akitumia jina la Daudi Albert Bashite.
Akihubiri huku waumini wake wakimsikiliza kwa umakini mkubwa, Mchungaji
Gwajima alisema kuwa, mwaka 2001, Makonda alitumia cheti cha mwanafunzi
huyo chenye divisheni 3 ya ponti 25 ili aweze kujiunga na Chuo cha Uvuvi
Nyegezi (NFTI) na ndiyo akaendelea hivyohivyo mpaka kufi ka Chuo Kikuu
cha Ushirika Moshi na baadaye kuingia kwenye siasa na leo hii ni Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam.
MAKONDA HAPENDWI?
Tangu kuingia kwenye siasa, Makonda amekuwa akikumbwa na ‘bahati mbaya’
ya kuwa na damu ya kunguni kiasi kwamba, kwa tafsiri ya kawaida ni
rahisi kusema kuwa, baadhi ya watu hawampendi lakini ni kutokana na
utendandaji wake uliotukuka.
AMANI LABAINI MAMBO 6 YANAYOMPONZA
Amani liliweza kuzungumza na baadhi ya watu kuhusu utendaji kazi wa
Makonda ambapo wengi walitoa maoni yao kwamba, yapo mambo
yaliyosababisha mheshimiwa huyo kuingia kwenye kuonekana na watu ‘ana
damu ya kunguni’ na ndiyo yanayomponza.
JAMBO LA KWANZA, WAKATI WA BUNGE LA KATIBA
Mwaka 2014, chini ya utawala wa Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’
Tanzania iliingia kwenye mchakato wa Katiba Inayopendekezwa ambayo Jaji
Joseph Warioba alikuwa mwenyekiti wa kutafuta maoni mitaani. Baada ya
maoni kukamilika, kulikuwa na mijadala mbalimbali ikiendelea, ikiwemo
kuundwa kwa Bunge la Katiba ambapo, Makonda alikuwa mmoja wa wajumbe
walioteuliwa na JK. Katika mjadala mmoja uliofanyika kwenye Jengo la
Ubungo Plaza jijini hapa na Jaji Warioba akiwa mshiriki mkuu, kulitokea
vurugu kubwa kiasi kwamba, mzee Warioba alidaiwa kupigwa.
Mengi yalisemwa, baadhi ya watu walidiriki kutamka kwamba, miongoni mwa
watu waliompiga mzee Warioba ni Makonda. Ilibidi Makonda atumie nguvu
kubwa kukanusha kwamba, yeye siye aliyempiga mzee Warioba bali
aliingilia kati kuamua na kumuweka sawa mzee huyo aliyewahi kuwa waziri
mkuu mwaka 1990.
Hata hivyo, licha ya utetezi wake, Warioba mwenyewe alitoa tamko kwamba
hakupigwa na Makonda, lakini watu walishindwa kumwelewa mzee huyo na
kuendelea na madai kwamba ni Makonda tu. Kuanzia hapo, jamii ilianza
kumuona Makonda kama si mjamii kwa tukio la kusema alimpiga mzee Warioba
na kukatokea mgawanyiko wa watu, waliomshabikia na waliokataa
kumshabikia ambao idadi yao kama iliuelemea mzani.
MKUU WA WILAYA
Nyota ya Makonda licha ya madai ya kumpa kichapo mzee Warioba, ilizidi
kung’ara, kufumba na kufumbua JK akampa ukuu wa wilaya ya Kinondoni
ambapo kwa hakika, alijitokeza mstari wa mbele kutatua migogoro ya ardhi
na kuonekana kwenye vyombo vya habari kila kukicha kwamba, anatetea
wanyonge. Wapo waliomkubali kwa kazi hiyo, wengine waliendelea kuwa na
msimamo uleule kwamba hawamkubali.
JAMBO LA PILI, NAULI ZA WALIMU DAR
Bado akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Makonda aliwahi kutoa ofa ya
walimu wa Jiji la Dar kupanda bure daladala. Lakini siku ya kwanza ya
zoezi hilo hakuna mwalimu aliyekubali kulipiwa nauli wakidai kuwa,
wanaweza kujilipia wenyewe. Nyuma ya zeozi hilo ilisemekana kuwa, walimu
waliwahi kukerwa na matamshi ya Makonda siku za nyuma kuhusu walimu na
madaraja yao ya kazi.
Kwa hiyo walimu nao wakamuona Makonda ni ‘adui’ yao. Mwaka 2015, mwaka
mmoja tu baada ya Bunge la Katiba, akaingia madarakani Rais Dk. John
Pombe Magufuli ‘JPM’ huku Makonda akiendelea kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni, lakini kabla ya kupepesa macho, JPM akamteua kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam ‘RC’. Hapo ndipo yakaongezeka mambo juu ya mambo.
JAMBO LA TATU, APIGA VITA SHISHA, MASHOGA NA MACHANGU
Makonda aliingia kwenye kiti cha u-RC akiwa na munkari wa kufanya kazi,
alihakikisha jiji linakuwa safi kwa wakazi wake kufuata maadili na
kuachana na maisha ya mkato. Kwa hiyo alipiga vita matumizi ya kilevi
aina ya shisha, akatangaza vita na wanaume tata ‘mashoga’ lakini pia
akawaambia wanawake wanaojiuza ‘machangudoa’ kwamba, waachane na
biashara hiyo mara moja.
Makundi ya watu yakaibuka na kudai; ‘Makonda anajifanya ni mchapakazi
sana ili rais ampende’. Kwa hiyo akaongeza sababu nyingine ya kuwa na
‘maadui’ kwani wavuta shisha walikasirishwa kwa kuondolewa kwa starehe
yao hiyo achilia mbali mashoga na machangu ambao walimuona anawakomalia
hivyo kuwahatarishia njia zao haramu za kupata kipato.
JAMBO LA NNE, ZOEZI LA DAR ES SALAAM MPYA
Siyo siri wala hakuna sababu ya kupepesa macho, miongoni mwa mambo
ambayo, yalimwongezea ‘maadui’ Makonda ni oparesheni ya Dar Mpya ambayo
aliifanya kwa nia njema ya kutatua matatizo mbalimbali ya wananchi wa
mkoa wake huo wenye watu karibu milioni 6. Zoezi hilo lilifanyika kwa
siku karibia saba ambapo Makonda na wasaidizi wake walikuwa wakifanya
mikutano ya hadhara kila siku katika maeneo mbalimbali na kusikiliza
kero.
Katika kusikiliza kero hizo baadhi ya watu, hasa viongozi wa serikali
za mitaa na wengine, walijikuta wakikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya kutuhumiwa hadharani.
Mbaya zaidi ili watuhumiwa hao wakamatwe, Makonda alikuwa akiamuru kwa
sauti na kuwanyooshea vidole mkutanoni huku kituo kimoja cha runinga
jijini Dar kikirusha mubashara matukio hayo hivyo wengi kudai ni
udhalilishaji.
Baada ya mikutano ya Dar es Salaam Mpya kumalizika, baadhi ya watu
walikuwa mahabusu, wengine mahakamani kwa tuhuma za matumizi mabaya ya
ofi si au pesa, lakini huku Makonda mwenyewe akiwa ameongeza idadi ya
‘maadui’.
JAMBO LA TANO, MATAMSHI YAKE
Katika mikutano hiyo, watu wengi walikuwa wakilalamikia kitendo cha
Makonda kuwasemea maneno makali viongozi waliokuwa wanatuhumiwa kwamba,
hakuwa anajali umri wao na hivyo kusema lolote lile.
“Kwenye ile mikutano ya Dar Mpya hakuna jambo lilikuwa likiniumiza kama
matamshi yake Makonda. Unajua wengine walikuwa sawa na wazazi wake,
lakini yeye akawa hachagui maneno ya kusema. Unajua ulimi siku zote
bwana ndiyo wenye kuleta tatizo.
“Ni vyema kiongozi akawa anaingiza maneno yake kwenye kipimo kwanza
kabla ya kutoa sauti. Kipimo cha kazi yake ni kuchuja, kwamba hili
niliseme, hili hapana,” alisema Hussein Mohamed, mkazi wa Buguruni na
kuongeza:
“Unajua inawezekana kabisa, kule kupendwa sana na rais ndiyo kumempa ‘kichwa’ cha kutoa kauli kali za namna ile.”
JAMBO LA SITA, MADAWA YA KULEVYA Licha ya kuacha ‘majeruhi’ kibao
kwenye zoezi la Dar Mpya, bado Makonda kama kawaida yake, hakuacha
kujipa ujasiri na kufanya kazi ya kutumikia wananchi na kupinga mambo
yaliyo kinyume na uadilifu, hivyo Februari 2, mwaka huu, Makonda kwa
mara ya kwanza na akiwa mkuu wa mkoa wa kwanza nchini, alijitokeza
hadharani na kutaja majina kadhaa ya watu aliodai wanajihusisha na
madawa ya kulevya.
Katika majina hayo, yalikuwepo ya watu maarufu, akiwemo Miss Tanzania
2006, Wema Sepetu na askari polisi 12. Makonda aliwataka watu hao kufi ka
kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Dar kwa mahojiano ambapo walitii.
Baada ya sakata hilo, Februari 8, mwaka huu, Makonda akaibuka na listi
kama siyo orodha ya watu wengine 65 akiwataja majina na kuwataka wafi ke
kwenye kituo hichohicho cha polisi kwa ajili ya mahojiano. Miongoni mwa
watu hao, walikuwemo wenye majina makubwa nchini kama vile,
mfanyabiashara Yusuf Manji, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (Chama
Cha Mapinduzi), Idd Azzan na Gwajima ambaye ndiye aliyeibua hoja ya
vyeti.
‘MAADUI’ WAONGEZEKA’ Kitendo cha Makonda kutaja majina ya wadaiwa
kujihusisha na madawa ya kulevya hadharani kiliibua hoja nyingine, wengi
walijitokeza wakipinga kwamba, hakuwa sahihi kwa sababu watu hao ni
watuhumiwa tu.
Hoja hiyo ilipaa juu zaidi hadi kufi kia kushika mjadala mkubwa nchini
kwamba ni sahihi au siyo sahihi? Miongoni mwa watu waliokereka na
kutajwa ni Gwajima.
Yeye alisema kuwa, Makonda alimtendea sivyo hivyo akatangaza vita naye.
Katika vita hiyo, ndipo Gwajima naye akadai amechimba na kuchimbua na
kubaini kuwa, Makonda alitumia vyeti vya mtu mwingine kuingia chuo baada
ya yeye kufeli hivyo akamtaka Rais Magufuli kumwajibisha.
NIA YAKE NI NJEMA
Katika mtazamo wa kawaida, katika yote aliyoyafanya au kuyasimamia
Makonda yana njia njema kwa jamii. Nani asiyejua madawa ya kulevya
yanavyoathiri jamii? Nani asiyejua shisha inavyoharibu vijana? Nani
asiyejua ukahaba unavyoweza kuleta magonjwa? Lakini pengine uwasilishaji
wake ndiyo umekuwa ukisumbua wengi.
NDIYO YAMEMPONZA
Makonda leo hii kama asingetaja hadharani majina ya watu wa unga, kama
asingejitolea kuwapiga vita machangu na mashoga, kama asingewakera
walimu kwa nauli, kama asingefanya mikutano ya Dar Mpya ina maana
angekuwa ni mkuu wa mkoa aliyepoa na kuonekana mwema machoni kwa watu.
Kumbukumbu ziko hivyo, wale wanaojitoa mhanga kusimama mbele za watu na
kupambana kwa dhati kukosoa matatizo hukumbwa na vita kubwa kutoka kwa
watu wenye
Tags
MAKONDA
