Mke wa Rais alipojua udhaifu wa mume wake, kwamba anampenda sana acha
afanye vituko. Nchi ikasimama. Vurugu zote yeye. Nani wa kumzuia na
ndiye usingizi wa Mkuu wa Nchi?
Watu waliufahamu ukali wa Rais lakini wakawa wanastaajabu ukimya wake
juu ya vitendo vya mkewe. Wengine wakasema Rais ni Bushoke, wapo
waliodai Rais huchimbwa mkwara wa kunyimwa unyumba ndiyo maana alikuwa
mpole.
Lucy Kibaki, Mungu amrehemu, aliitikisa Kenya miaka 10 ya Urais wa mume wake, Mwai Kibaki, kati ya mwaka 2002 mpaka 2012.
Lucy hakuwa wa mchezo, alivamia chombo cha habari na kushambulia
wahariri. Aliwahi kumpa makofi mpiga picha wa gazeti la Nation kwenye
kadamnasi. Watu wakashangaa. Mume wake akawa kimya.
Mwaka 2007, katika sherehe ya Siku ya Jamhuri, iliyofanyika Ikulu, MC
alimtambulisha Lucy Kibaki kwa majina ya Lucy Wamboi Kibaki badala ya
Lucy Muthoni Kibaki, basi MC mbele za watu akachezea makofi.
Kibaki alishuhudia lakini afanye nini? Lucy ndiye usingizi wake. Mama
akazidi kutamba, akamtwanga makofi mtumishi wa Ikulu, Matere Keriri.
Halafu akatamba: “Nikisema mimi ndiyo sauti ya mwisho.” Usimchezee mama
Prezidaa!
Bunge la Kenya likachachamaa na kumsema Kibaki kwa kushindwa kumdhibiti
mkewe. Lucy akamwambia mwanasheria Gitobu Imanyara, afungue kesi dhidi
ya wabunge. Imanyara aliposema mashitaka yasingekuwa na nguvu, alichezea
makofi.
Kibaki alikuwa na kawaida ya kuwaalika marafiki zake na kupata mvinyo
kwenye baa ya Ikulu. Lucy akatimua marafiki wa Kibaki halafu akaagiza
baa ifungwe.
Kipindi fulani vyombo vya habari viliripoti Kibaki alikuwa na mke
mwingine tofauti na Lucy, basi mama akachachamaa, akamwagiza mumewe
afanye mkutano na waandishi wa habari ili akanushe. Kibaki alikanusha
huku Lucy akimsimamia.
HATA MAREKANI
Rais wa 19 wa Marekani, Warren Harding naye alikuwa mnyonge kwa mkewe,
Florence Harding. Wakati huo, mpaka magazeti yaliandika kuwa nchi
ilikuwa na inaongozwa na First Lady.
Florence aliagiza intelijensia kufanya kazi, alimwandikia Rais Harding
cha kuzungumza kwa waandishi wa habari. Florence ndiye alikuwa kila kitu
kwa Serikali ya Marekani. Florence aliwahi kusema yeye ndiye sauti ya
Rais. Ni kama mtu mzima Robert Mugabe alivyo mpole kwa Grace.
Unajua jeuri yote ya nini? Ni mke kujua anapendwa. Mke wa Rais asiye na
busara akishajua mume wake amependa mpaka ameoza kwake, basi hufanya
vituko mpaka kumdhalilisha Rais mwenyewe na nchi yote.
Author: Luqman MALOTO
Tags
MKE WA RAIS
