BANDA MEDIA BLOG

MWENYEKITI WA JUMUIA YA WAZAZI AWATAKA WANAOTAKA KUGUMBEA UONGZI KUJIPIMA


MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Abdallah Bulembo amewataka wajumbe wa Jumuiya hiyo wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali ndani ya Jumuiya kujipima kama wanastahili kushika nafasi hizo huku akisema,yeye hatagombea tena nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Bulembo alitoa kauli hiyo jana muda mfupi kabla ya kufungua kikao  cha dharura cha Baraza hilo lililofanyika mjini hapa huku akisema kuwa,wale wote waliokuwa viongozi wanaweza kuchaguliwa iwapo wamefanya vizuri katika vipidi vyao ndani ya  miaka mitano iliyopita.

“Hiki ni kikao muhimu kwa Jumuiya ya Wazazi na Chama kwa ujumla,ni mwaka wa uchaguzi ,kama ulifanya vizuri ndani ya mkoa wako ,utachaguliwa, na kama ulifanya vibaya tambua kuwa huchaguliki,jalamba lako ni kujipima tu ,uliyafanya yapi,na  mema  yapi yanakurudisha.

“Msiende kuwafanyia figisu watu wanaotaka kuwaondoa kwenye nafasi zenu ,msiende kuwafanyia ubaya kwa sababu wakati ninyi mnaingia kwenye nafasi mlizo nazo ,pia zilikuwa na watu .”alisema Blembo

Alisema,kuna baadhi ya viongozi hususani wenyeviti ,wamekaa kwenye nafasi zao kwa kipindi cha miaka mitano lakini hawajawahi kuitisha vikao na waliojitahidi wameitisha kikao kimoja ama vikao viwili.

“Kwa nini unachaguliwa tena,wakati taarifa za wilaya na mkoa zikihitajika  hazipo makao makuu, jipime kama unayo haki ya kuchaguliwa kuitumikia Jumuiya,kama huna haki ,usiwawekee watu zengwe,maana waliokupigia kura ndio wanakupima wewe,

“Nayasema haya kwa kuwa vikao vijavyo ni vya kujadili majina yenu (wagombea),mimi mwaka huu sigombei tena,miaka yangu mitano imefika mwisho, narudi kijijini kwangu ,kwa hiyo ndani yenu wenyeviti msije mkaulizana maswali ,wenye kutaka kuwa wenyeviti wa Jumuiya ya wazazi ni wakati wenu ,usitengeneze wasiwasi wala usiulize kwa nini.”alisema


Bulembo aliwataka wanaotaka kugombea wasimshirikishe kwa lolote isipokuwa wakati ukifika wakachukue fomu na kwamba atakutana na majina yao kwenye vikao maamuzi na siyo vinginevyo.
“Na kwamba asitokee mtu kwenda kuomba kura kwa wajumbe akidai amekubaliana na mimi kwamba agombee nafasi hiyo.


Mwenyekiti huyo alisema,anaondoka katika nafasi yake akiwa ametekeleza kwa asilimia 75 yote aliyoahidi miaka mitano iliyopita wakati alipokuwa akigombea nafasi hiyo.

“Tuliamua kuacha kazi zetu tukafanya kazi za chama na Jumuiya yake,Jumuiya imebadilika ,sikuikuta hivi ,mimi  tangu nimeingia kwenye uongozi hatujawahi kuomba fedha kwa ajili ya vikao vya Jumuiya.”

Akizungumzia kuhusu Bulembo kutogombea tena nafasi ya uenyekiti,Mjumbe wa Jumuiya hiyo kutoka mkoa wa Pwani Karu Karavani alisema uamuzi wa mwenyekiti kutogombea tena nafasi hiyo ni uamuzi wa busara .

“Kutokana na Bulembo kuteuliwa kuwa Mbunge ,labda ameona atakuwa na shughuli nyingi ambazo zitamsababishia kushindwa kutekeleza ipasavyo shughuli za Jumuiya”alisema .

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG