Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye amemtaka
Mkurugenzi wa Habari maelezo kufuatilia utendaji kazi wa maafisa habari
na mawasiano wote ili kuona utendaji kazi wao kama unaleta maendeleo
kwa jamii.
Waziri huyo ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na maafisa habari
na mawasiliano wakati akifungua kikao kazi cha 12 cha Maafisa
Mawasiliano wa Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo
Mkoani Dodoma.
Amesema kuwa wao ndiyo chanzo cha kuwafanya viongozi wao kukimbia vyombo
vya habari kutokana na maafisa hao kushindwa kuwaandaa vyema badala ya
kutoa habari zinazotakiwa kwa jamii.
Amesema kuwa maafisa habari na viongozi wa umma nchini wanapaswa
kutekeleza sheria hasa zinazowataka kutoa habari na taarifa kwa
kuhakikisha vyombo vya habari na wananchi wanapata habari kwa wakati
bila urasimu.
“Nataka niiagize ofisi ya mkurugenzi wa habari maelezo kuhakikisha kuwa
mnafuatilia utendaji kazi wa kila afisa habari na mawasiliano ili
kujiridhisha kama wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria au la na kama
tutabaini kuna afisa habari ambaye hatekelezi majukumu yake ipasavyo
tumuombe atupishe”. Alisema Nape
Aidha Waziri huyo aliwasisitizia maafisa hao kutoa ushirikiano mzuri kwa
waandishi wa habari pindi wanapofika katika ofisi zao kuwapa taarifa
sahihi na kwa wakati ili jamii iweze kupata ufumbuzi ya matatizo yao.
Tags
Nape Nnauye
