Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Shehena ya pombe kali
zilizofungwa katika vifungashio vya plastiki (Viroba) zenye thamani ya
shilingi bilioni 2 zimekamatwa Jijini, Dar es Salaam katika operesheni
inayoendelea ya kuondoa pombe hizo nchini.
Mwanasheria wa Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Manchale Heche ameyasema hayo
leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika
operesheni hiyo ambayo inaendelea kwa nchi nzima.
“Bado tunaendelea na operesheni
ya ukamataji na uzuiaji wa pombe za viroba, ambapo leo katika ghala la
kampuni ya Lovekira iliyoko Tegeta, Wazo tumefanikiwa kukamata zaidi ya
katoni 7000 za pombe za viroba aina ya Konyagi, Valeur, Burudani na
Zanzi ambazo ujazo wake ni kati ya mililita 50 mpaka 200,” alifafanua
Heche.
Aliendelea kwa kusema kuwa, licha
ya shehena ya viroba iliyokutwa katika ghala hilo bado kampuni hiyo
inaendelea kuingiza mizigo ya viroba ambapo timu iliyofika kukagua ghala
hilo ilikuta katoni nyingine za pombe hizo zikiwa ndani ya gari
zikisubiri kuingizwa ndani ya ghala hilo.
Kwa upande wake Meneja wa kampuni
hiyo Siah Mboya amesema kwamba, viroba vilivyokuwa ndani ya gari
vilikuwa vikihamishwa kutoka tawi lingine la kampuni hiyo lililoko
Tegeta kutokana na Serikali kusitisha uuzaji na usambazaji wa pombe
hizo.
Aliendelea kwa kusema kuwa
wamekuwa na shehena kubwa ya pombe hizo kutokana na kuwa na mzigo mkubwa
ulionunuliwa kati ya mwaka 2014 hadi 2015. Aidha ameiomba Serikali
kuongeza muda wa matumizi ya pombe hizo ili waweze kumaliza mzigo ambao
bado upo katika maghala.
Nae, Afisa Afya wa Manispaa ya
Kinondoni John Kijumbe amesema kwamba, baada ya kutambua idadi ya pombe
za viroba iliyokamatwa. Muhusika wa mzigo uliokamatwa pamoja na Afisa wa
Serikali husaini fomu inayotaja kiasi cha pombe kilichokamatwa na
kupewa maelekezo ya kutoondoa mzigo huo mpaka Serikali itakapotoa
maelekezo.
Operesheni ya kuondoa pombe za
viroba ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la
kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hizo
kuanzia Machi 01, 2017.
Aidha pombe hizo zimechangia kwa
kiwango kikubwa uchafu wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa,
ajali na vifo vilivyosababishwa na unywaji uliokithiri wa pombe hizo,
kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kupotea kwa mapato
yanayosababishwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Tags
POMBE ZA VIROBA