Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amezungumzia suala la marafiki
zake kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya huku akisisitiza kwamba
wanaodaiwa kuwa ni marafiki zake sio bali ni watu anaokutana nao katika
maeneo anayotembelea.
Mbunge huyo amezungumza hayo jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa
na Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya nchini, ambapo
alisema roho yake imesuuzika kwani jamii imeamini kwamba hahusiki kwa
namna yoyote ile na biashara hiyo haramu.
Ridhiwani alieleza kufurahishwa kwake baada ya kuhojiwa na Mamlaka hiyo nchini.
“Nashukuru kwa kuhojiwa huku nimepata nafasi ya kueleza ukweli juu ya
jambo hili ambalo lilishaanza kuleta taharuki katika jamii, sasa umma
umejua kuwa siuzi wala sihusiki na dawa za kulevya, roho yangu
imesuuzika,” alisema Ridhiwani.
Alisema vita ya dawa ya kulevya ni kubwa na inapaswa kupigwa na kila
mmoja ili kuokoa kundi kubwa la vijana ambao wanaathirika kutokana na
suala hilo na kwamba kuhojiwa kwake kumemfanya awe na amani.
“Naunga mkono vita hii ya dawa za kulevya nchini kwani itasaidia
kurudisha nguvu kazi inayopotea kutokana na matumizi ya dawa hizo za
kulevya kwa mzazi ambaye mtoto wake ameathirika na matumizi ya dawa hizo
anajua uchungu wake na hasara zake,” alisema Ridhiwani.
Aidha, aliongeza kuwa jamii inapaswa kusimama kwa kauli moja ili
kuliokoa Taifa na nguvu kazi inayopotea ili Taifa liwe na vijana
wanaojitambua na kutimiza wajibu wao katika kulitumikia taifa.
Ridhiwani alisema mchakato huo wa kupambana na dawa za kulenya nchini
umekuwa ukiwachanganya wananchi kwani haieleweki ni nani anayehusika na
kushugulikia suala hilo.
“Huu mchakato umekua ukichanganya, kuna watu wanaitwa kwa Kamanda Sirro
na wengine wanaitwa kwa Kamishna Sianga (Rogers), mfano msanii Vanessa
Mdee ambaye ameitwa kwa Kamanda Sirro badala ya kwa Kamishna Sianga,”
alisema Ridhiwani.
Alisema watu wanahoji kwanini wengine watangazwe hadharani na wengine
kuitwa kimya kimya na ameongeza kuwa ni vyema mamlaka zikajipanga ili
kufanikisha vita hii na kufikia malengo yake ya kumaliza tatizo la dawa
za kulevya nchini
Tags
MADAWA YA KULEVYA
