Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Afya kutoka nchini Kenya Dkt. Cleopa Mailu wakimsikiliza
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza kuhusu Kutangaza ajira
za Madaktari wapatao 500 ambao watakwenda kufanya kazi nchini Kenya.
Ajira hizo zitawahusu Madaktari ambao hawajaajiriwa Serikalini(hawapo
katika utumishi wa umma au taasisi za serikali. PICHA NA IKULU
…………………………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika na Jovina Bujulu-MAELEZO
Dar es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania imekubali ombi la Serikali ya Kenya la kuwapatia madaktari
500 kufuatia upugufu wa madaktari uliotokana na mgomo nchini humo.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kutoka na maombi
yaliyotolewa, serikali imeandaa utaratibu kwa madaktari wa kitanzania
kuwasilisha maombi yao katika tovuti ya wizara ya afya pamoja kufuata
taratibu zingine kama watakavyoelekezwa.
Alizitaja sifa za anayetakiwa
kuomba nafasi hiyo kuwa ni shahada ya kwanza ya udaktari, mafunzo ya
vitendo pamoja na kusajiliwa na Baraza madaktari la Tanganyika na
kutuma maombi hayo katika barua pepe; maombiyakazi@moh.go.tz kabla ya Machi 27saa 10 jioni.
Aidha, waombaji wanatakiwa
kuambatanisha wasifu wao, nakala za vyeti vya taaluma na matokeo, cheti
cha kuzaliwa, cheti cha kuhitimu mafunzo kwa vitendo pamoja na cheti
cha usajili kutoka Baraza madaktari la Tanganyika.
“Tanzania hatuna upungufu wa
madaktari isipokuwa Serikali haina uwezo wa kuajiri madaktari wote
wanaohitimu, kwa kuwa kwa mwaka kuna wahimu 1200 wa shahada ya kwanza ya
udaktari na uwezo wa kuajiri ni 450 tu” alisema Ummy
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema
kuwa ajira hizo hazitawahusu watumishi wa umma, hospitali teule za
halmashauri na mashirika ya hiari ambao wanalipwa mshahara na serikali.
Madaktari watakaokidhi vigezo na sifa watapewa mkataba wa ajira wa miaka
miwili.
Nchi ya Kenya inakabiliwa na
upungufu wa madaktari kutokana na mgomo ulioanza mwezi Desemba mwaka
jana, ambapo madaktari hao wamekuwa wakaidai nyongeza ya mshahara na
marupurupu mengine.
Tags
AJIRA