Wizara
ya Nishati na Madini inapenda kuujulisha Umma, Kampuni na watu
wanaojihusisha na uvunaji wa madini nchini, kuwa usafirishaji wa
makinikia (concentrates) na mawe yeye madini (ore) ya metallic minerals kama
vile dhahabu, shaba, nikeli na fedha umesitishwa kuanzia tarehe 02
Machi, 2017.
Usitishwaji huu unalenga kuhakikisha kuwa madini
yanayochimbwa hapa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa
kwenda nje hasa kwa ajili ya uyeyushaji (smelting) na usafishaji (refining)
ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Sheria ya
Madini ya Mwaka 2010. Aidha, shughuli za uongezaji thamani madini hapa
nchini zitatoa fursa ya ajira, mapato na kuhawilisha teknolojia na hivyo
kuleta manufaa zaidi kwa Taifa.
Hivyo, ni mategemeo yetu kuwa
Kampuni na watu wote wanaovuna madini nchini ambao walikuwa
wanasafirisha makinikia ya madini pamoja na mawe yenye madini
watazingatia ipasavyo kutosafirisha tena kwenda nje ya nchi kwa ajili ya
uyeyusahji na usafishaji. Wanatakiwa kuanza taratibu za kufanya
shughuli hizo hapa nchini. Serikali itatoa ushirikiano unaotakiwa kwa
Kampuni au watu watakaojishughulisha na shughuli za uchenjuaji madini
hapa nchini hasa uyeyushaji na usafishaji wa madini.
Imetolewa na ;
KATIBU MKUU
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
3 Machi, 2017