
[Sehemu ya 1 ya Hotuba ya ndugu Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto (MB)
kuhusu Mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na Bajeti ya Ofisi ya
Waziri Mkuu Kwa mwaka 2017/18]
Mheshimiwa Spika,
Tangu mwezi Novemba mwaka 2015 nchi yetu ilipata Serikali mpya iliyoanza
kazi kwa kasi kubwa haswa katika maeneo ya kupambana na rushwa, ufisadi
na kuongeza mapato ya Serikali. Wananchi walikuwa na matumaini makubwa
sana kutokana na mwanzo huu, na hata ufanisi katika utendaji wa kazi
Serikalini ulianza kuboreka.
Bahati mbaya, leo tunapokutana kujadili utendaji wa Serikali wa mwaka
uliopita na kupanga Bajeti ya mwaka unaofuata wa fedha matumaini hayapo
tena, kuna hali kubwa ya kukata tamaa miongoni mwa wananchi.
Maeneo mengi ya nchi kuna uhaba mkubwa wa chakula na badala ya Serikali
na hasa Rais kuwa matumaini Kwa wananchi akiwa Comforter In Chief,
kumekuwa na maneno makali ya kuwakatisha tamaa wananchi. Bei za vyakula
nchini zimepanda mno kiasi cha wananchi kushindwa kumudu chakula ili
waweze kufanya kazi na kukuza Uchumi.
Taarifa za Serikali kupitia ripoti za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti
yake juu ya hali ya Uchumi ya nchi yetu (Quartely Economic Review na
Monthly Economic Review) kwa mwezi wa Disemba 2016 zinaonesha kuwa kuna
mfumuko mkubwa mno wa bei za Vyakula, hasa Chakula Kikuu kwa Watanzania -
Mahindi, ambapo bei ya chakula hicho kikuu nchini imepanda kwa zaidi ya
30% na kupandisha mno gharama za maisha za wananchi wote nchi nzima.
Leo bei ya kilo moja ya mahindi nchini iko sawa au ni zaidi ya bei ya
kilo moja ya mchele kwenye miji mbalimbali nchini, sukari bei juu,
mafuta ya kula bei juu nk. Kwa wakazi wa mjini hata bei ya gesi kwaajili
ya kupikia majumbani imepanda, wananchi wamerudia matumizi ya mkaa,
tujiandae na uharibifu wa misitu nchini.
Jana Ofisi ya takwimu ya Taifa imetoa Taarifa ya kuonyesha kuwa Mfumuko
wa Bei umepanda kwa kasi na sasa umefika asilimia 6.4 Kwa mwaka
unaoishia Machi, 2017. Ibara ya 20 ya Hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa
bungeni inaonyesha mfumuko wa bei wa asilimia 5.2 kwani wametumia
takwimu za mwezi Desemba, 2016.
Ukuaji wa sekta binafsi umedorora na kushuhudia biashara maelfu kwa
maelfu zikifungwa na kusababisha ajira nyingi kupotea na ajira chache
kutengenezwa. Katka Ibara ya 26 ya Hotuba ya Waziri Mkuu inaonekana kuwa
ajira 418,000 zilizalishwa mwaka 2016/17. Lakini Waziri Mkuu
hakulieleza Taifa kuwa Hivi sasa Watanzania 1.6m wanaingia kwenye soko
la Ajira kila mwaka. Pia Waziri Mkuu hakueleza Taifa ni ajira ngapi
zimepotea Kwa viwanda kufungwa au kupunguza uzalishaji na biashara
kufungwa. Manispaa ya Ilala peke yake imefunga biashara 2900 na hivyo
kupoteza chanzo cha mapato ya Manispaa. Lakini hata mikopo ya Kibenki
kwa sekta binafsi imepungua mno, ikiwa ni kiashiria cha mdororo wa sekta
binafsi.
Matamko ya viongozi wakuu wa Serikali kuhusu mwelekeo wa Uchumi yanatuma
ujumbe hasi kuhusu uwekezaji wa mitaji nchini, na hivi sasa kila
mwekezaji kwenye macho ya Serikali anaonekana mpiga dili. Juhudi zote za
kuhamasisha uwekaji wa mitaji nchini zilizofanywa tangu Serikali ya
awamu ya tatu, zimefutwa katika mwaka Mmoja tu wa Serikali ya awamu ya
tano. Hali ni ya kusikitisha sana.
Tatizo jengine kubwa ni suala la ajira, ukiondoa ajira zilizopotea kwa
mdororo wa sekta binafsi, lakini pia hakuna ajira mpya serikalini tangu
awamu ya tano iingie madarakani. Vijana mbalimbali waliomaliza masomo
yao ya Ualimu, Utabibu, Maafisa Kilimo, Mifugo na Uvivu bado wako mtaani
bila ajira kwa mwaka sasa. Hata walioajiriwa mwanzoni ajira
zilisitishwa kwa kisingizio cha uhakiki wa watumishi wa Umma.
Yote hayo yana athari kwenye uchumi wa nchi, yamepunguza kipato cha
wananchi, yamechangia ugumu wa maisha. Yamefuta matumaini waliyokuwa
nayo watanzania na yamewakatisha tamaa. Bunge letu lina wajibu wa
kuhakikisha Serikali inarelebisha hayo.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge - Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Bungeni Dodoma
April 11, 2017
Tags
Zitto Kabwe