Benny Mwaipaja-WFM, Dodoma
Mikoa mitatu ya Tanga, Morogoro na
Iringa, imenufaika na kiasi cha shilingi bilioni 6.5 zilizotolewa kama
mkopo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) tangu benki hiyo ianzishwe
mwaka 2015.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni
Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji,
wakati akijibu swali na msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu,
Mhe. Felister Aloyce Bura, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza
kutoa huduma kwa wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Dodoma.
Dkt. Kijaji ameeleza kuwa hadi
kufikia mwezi Desemba, 2016, TADB imetoa mikopo ya jumla ya shilingi
6,489,521,120 kwa ajili ya kutekeleza miradi ishirini (20) ya kilimo
katika mikoa hiyo mitatu ya Iringa, Morogoro na Tanga.
“Sambama na utoaji mikopo, Benki
inatoa mafunzo kwa wakulima ambapo hadi sasa vikundi 336 vya wakulima
wadogowadogo vyenye jumla ya wanachama 44,400 wamepatiwa mafunzo hayo
katika mikoa hiyo mitatu” aliongeza Dkt. Kijaji
Amesema kuwa Benki hiyo inatarajia
kuanza kutoa huduma hiyo kwa wakulima wadogowadogo wa Mkoa wa Dodoma na
mikoa mingine jirani wenye sifa.
“Benki imepata nafasi kwa ajili ya
kufungua ofisi katika jengo la PSPF mjini Dodoma na itakabidhiwa ofisi
hiyo mwezi Julai, 2017, baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi wa jengo
hilo” Alisisitiza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji amesema kuwa tayari
Benki hiyo imemwandikia barua Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma ili kuomba
aipatie miradi mizuri ya kilimo ambayo mkoa unapendekeza Benki
iifikirie katika zoezi la kutoa mikopo itakayoanza kutolewa mwishoni mwa
mwaka 2017.
Tags
TADB BENKI