Mwenyekiti wa CHADEMA na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Mh
Freeman Mbowe amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuacha kuwachagulia
viongozi.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana bunge kupiga kura za hapana kwa
wagombea wa CHADEMA ambao walipaswa kuwa wawikilishi waTanzania katika
Bunge la Afrika Mashariki na kusema wapende wasipende nafasi hizo mbili
za CHADEMA zipo pale pale, huku akitangaza kuwa chama hicho kitakwenda
mahakamani kudai haki.
"CHADEMA tutakwenda kuitafuta haki pengine, kama taifa tungetegemea
kupata wawakilishi na tuwe tumemaliza uchaguzi huu wa kuwapata
wawakilishi wetu kwenye Bunge la Afrika Mashariki, lakini ndiyo kwanza
kwa matokeo haya na kwa utaratibu huu wa upindishaji wa sheria za
uchaguzi, tutakwenda mahakamani, tutaitafuta haki hii mahali pengine"
alisema Freeman Mbowe
Mbali na hilo kiongozi huyo amesema ni jambo lisilowezekana kwa chama kimoja kuwapangia wapinzani kiongozi wamtakao wao.
"Ni aibu kwa taifa kwamba chama kimoja kinataka kutafuta na kupitisha
mgombea wa chama kingine cha upinzani, haiwezekani na haikubaliki, Spika
amevunja kanuni za Bunge, sheria hazikuheshimiwa, ubabe umetumika
lakini kwetu sisi ni sehemu ya mchakato wa demokrasia tutaendelea
kuitafuta haki yetu". Alisema Mbowe
Kuhusu nafasi zao, Mbowe amesema, "Nafasi mbili za Ubunge wa Bunge la
Afrika Mashariki wapende wasipende ni za CHADEMA, tutakaa tutashauriana,
hawawezi kueleza sababu za msingi za kuwakataa wagombea wetu. Kwa
sababu wagombea wetu wana sifa, lakini tunajua huu ni mkakati wa CCM ,
Rais anahusika, Waziri Mkuu anahusika na viongozi wao wanahusika.
Wanatumia Sheria gani kutuchagulia wapinzani wawakilishi wetu katika
Bunge la Afrika Mashariki? Alihoji Mbowe. "
